Header Ads

ad

Breaking News

JKCI kutoa matibabu ya Kibingwa ya moyo Visiwa vya Comoro

Na Mwandishi Wetu

KUNDI lingine la madaktari bingwa wa maradhi mbalimbali wameondoka nchini kwenda Comoro kwaajili ya kambi ya matibabu ya wiki moja visiwani humo.

Ujumbe wa Tanzania unajumuisha madaktari, wauguzi na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya unafikia watu 52 na waliondoka jana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air.

Kambi hiyo ya wiki moja inafuatia ombi lililotolewa na nchi hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipotembelea nchi hiyo mwaka huu wakati wa sherehe za miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo.

Madaktari hao ni kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma na maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Mkurugenzi Mkuu wa JKCI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Utalii Tiba, Dk Peter Kisenge alisema wanakwenda Comoro kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini humo mwaka huu wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wao.

“Madaktari waliokwenda Comoro Desemba mwaka jana Desemba walihudumia wananchi 2,700 na kati ya hao 271 walipata rufaa ya kuja Tanzania na walikuja hapa nchini tunashukuru sana mwitikio ulikuwa mkubwa na ndipo Rais wa Comoro alipomwomba Rais Samia turudi tena kule,” alisema

“Tunakwenda Comoro chini ya kitu tunaita tiba mkoba ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo tumezunguka mikoa mbalimbali nchini na sasa inavuka mipaka kwenda Comoro, Malawi, Congo na Burundi, nia ya kuvuka mipaka ni kuzieleza nchi zingine uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita,’ alisema Dkt. Kisenge.

Aidha, alisema serikali ya awamu ya sita imewekeza kwenye vifaa tiba na rasilimali watu kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba mataifa mengi yanakuja kujifunza mambo mbalimbali kuhusu tiba.

“Tumepeleka madaktari bingwa wabobezi, watu wa maabara, wauguzi tutatoa huduma ya matibabu ya aina mbalimbali na wapo wagonjwa watahitaji kuja kwa matibabu nchini Tanzania, watakaoletwa huku wataleta pesa za kigeni ambazo zitawanufaika watanzania kwa miradi ya maendeleo,” alisema

Alisema wanamikakati ya kwenda nchi mbalimbali kwa ajili ya kutoa tiba kama Afrika ya Kati DRC Congo na visiwa vya Shelisheli na kwamba dhamira ya Rais Samia ni kuongeza diplomasia kupitia utalii tiba.


No comments