Header Ads

ad

Breaking News

Mchechu achangisha milioni 117.8 ujenzi Kanisa Naibili

Msajili wa Hazina na kiongozi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya nyumba, benki na biashara, Bw.Nehemiah Mchechu (kulia), akizungumza jambo na Askofu Dkt.Fredrick Shoo, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Oktoba 20,2024 mkoani Kilimanjaro. 

Na Mwandishiu Wetu, Kilimanjaro

MSAJILI wa Hazina na kiongozi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya nyumba, benki na biashara, Bw.Nehemiah Mchechu ameendesha harambe iliyowezesha kuchangisha shilingi mlioni 117.8 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha mkoani Kilimanjaro.

Kati ya fedha hizo kwa ajili ya jengo hilo mpya la ibada ambalo ujenzi wake ulianza miaka sita iliyopita, shilingi milioni 50.2 ni taslimu, shilingi milioni 66.5 ni ahadi na sh milioni 1.1 zilipatikana kwa njia ya mnada.Katika harambe hiyo iliyofanyika Jumapili Oktoba 20, 2024), pia ilipatikana mifuko 118 ya saruji.

Fedha hizo na saruji ni kwa ajili ya upauzi wa jengo hilo la ibada na kazi ya plasta, kwa mujibu wa Askofu Dkt.Fredrick Shoo, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT. Kazi hizo mbili za upauzi na plasta, zinatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 150.

Akizungumza na viongozi wa kidini, serikali, kijamii na waumini wa Naibili, Bw.Mchechu alieleza haja ya kuendelea kuwa na moyo wa kutoa na kushirikiana mpaka ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada utakapokamilika.

Kwa sasa tayari jiwe la pembe limewekwa katika kanisa hilo, huku Bw. Mchechu akiwataka Wakristo kutoishia kwenye hatua hiyo ya kuweka Jiwe la Pembe tu.

“Tunapoendelea na ujenzi huu, nataka niwaombe ninyi wapendwa msiishie hapa. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja mpaka ujenzi utakapokamilika,” alisema.

Aliongeza; “Kanisa bado linahitaji michango yenu, maombi yenu, na utayari wenu wa kujitoa. Kila mmoja wetu anaweza kutoa kitu, iwe ni fedha, muda au huduma kwa namna yoyote ile.”

Alisema ikiwa watatoa kwa moyo wa upendo, Mungu atarudisha zaidi na zaidi na vikombe vyao vitafurika.

Bw.Mchechu alisisitiza kwa kunukuu Biblia katika Luka 6:38: "Wapeni watu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa, cha kusukwasukwa, na kushindiliwa, na kufurika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu."

Aliongeza; “Kama vile Nehemia alivyowaongoza watu wa Yerusalemu kujenga tena ukuta wa mji baada ya kuharibiwa, ninyi pia muendelee kujitoa kwa uaminifu na bidii katika ujenzi wa nyumba ya Mungu.”

Kwa upande wa Dkt.Shoo, alisema matamanio yao ni kuona wanakamilisha plasta, kuweka madirisha, milango na madhabahu, kupaka rangi na kuanza maandalizi ya kutengeneza samani, ifikapo mwaka 2026.

Mpaka kufikia hatua ya kabla ya upauzi, jumla ya shilingi milioni 229.8 zimetumika, shukrani kwa watu wenye mapenzi mema na Mungu kwa michango yao.

Askofu Shoo alisema baada ya upauzi na plasta, awamu ya pili ni kujenga madhabahu, madirisha na milango ya mbao.

Baada ya hapo awamu inayofuata itakuwa kuweka tarazo, bodi ya dari, kusuka umeme na rangi, huku awamu ya nne ikiwa ni kuweka viti na kumalizia madhabahu kwa kutumia mbao.

Alisema awamu ya mwisho itakuwa ni kufunga vifaa vya muziki, mifumo ya CCTV Kamera, kiyoyozi na mfumo wa TEHAMA.

“Ni wakati mwafaka wa kushirikiana kufanya kazi hii ya baraka iliyopo mbele yetu. Mungu atutie nguvu,” alihitimisha Askofu Dkt.Shoo.

Msajili wa Hazina na kiongozi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya nyumba, benki na biashara, Bw.Nehemiah Mchechu akizungumza na waumini wa Kanisa la KKKT Usharika wa Naibili, Siha mkoani Kilimanjarom wakati wa harambee ya kuendeleza ujenzi wa kanisa Oktoba 20,2024.

Askofu Dkt.Fredrick Shoo, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), akisalimiana na Msajili wa Hazina na kiongozi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya nyumba, benki na biashara, Bw.Nehemiah Mchechu

Msajili wa Hazina na kiongozi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya nyumba, benki na biashara, Bw.Nehemiah Mchechu akipokea shada la maua

No comments