MwanaFA: Wachagueni wagombea wa CCM
* Asema mapenzi ya vyama yasiyafanywe ushabiki wa Simba na Yanga
Mbunge wa Muheza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma 'MwanaFA'Na Mwandishi Wetu, Muheza
MBUNGE wa Muheza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma 'MwanaFA', amewataka wananchi wilayani Muheza mkoani Tanga Novemba 27, wachague wagombea wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ili kazi ya kuleta maendeleo iwe rahisi.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Tarafa ya Bwembera, MwanaFA amesema tangu kuanzishwa kwa CCM, imekuwa ikichaguliwa kwasababu ndiyo chama chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea watanzania maendeleo.
Amewataka wananchi waendelee kukiamini chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024 kwa kuwachagua wagombea wa chama hicho.
Amesema kamwe wasifanye mambo ya vyama kama ushabiki wa timu za mpira wa miguu za Simba na Yanga, kwani uchaguzi ni maisha ya watu na jukumu la viongozi ni kuleta maendeleo.
Amewakumbusha wananchi wa Muheza kwamba, tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo mwaka 1974, hakuna wakati wowote ule ambao serikali imeweza kugharamia miradi pamoja na kuleta fedha za maendeleo kama utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2024.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miaka minne ameweza kuleta fedha nyingi ambazo zimegharamia miradi ya elimu, afya, barabara, umeme pamoja na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.
MwanaFA amesema wakati akiingia kuwa mwakilishi wa Jimbo la Muheza mwaka 2020, wilaya hiyo ilikuwa haina shule za sekondari katika kata 13, lakini hivi sasa zimebaki kata mbili tu ambazo hadi kufikia 2025 zitakuwa zimejenga shule hizo.
Anatoa mfano kwamba, kwa miaka minne tangu Rais Dkt.Samia aingie madarakani, wamejenga vyumba 211 vya madarasa ya shule ya msingi na vyumba zaidi ya 100 vya shule ya sekondari, tofauti na utekelezaji wa ilani ya mwaka 2015-2020, ambapo kwa miaka mitano ilani ya uchaguzi ilitekeleza ujenzi wa vyumba 20 vya madarasa ya shule za msingi.
Kwa upande wa afya, MwanaFA amesema kulikuwa na kituo cha afya kimoja cha Mkuzi, lakini sasa wamepewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.1 kujenga vituo viwili, ambapo kimoja tayari kimejengwa Kata ya Kwafungo kwa gharama ya shilingi milioni 500.
Amesema kituo kingine kitajengwa katika Kijiji cha Mgambo Kata ya Misalai, ambapo hadi sasa wana kiasi cha shilingi milioni 649, pia wamepata hati miliki kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili wakamilishe kituo cha afya Ubwari kilichopo mjini Muheza.
"Ndugu zangu wa Muheza, Novemba 27 nendeni mkapige kura mkiwa kifua mbele kama mmepigwa ngumi za mgongo, mwende kuwachagua wagombea wa CCM kwasababu kazi imefanyika kwa kiwango kikubwa,"amesema MwanaFA.
"Mheshimiwa Rais anadhamira njema kabisa na watanzania na anatoa fedha hizo kuturahisishia maisha, ili wananchi wenzangu tuwe na maisha ya uhakika, maisha ya leo yawe rahisi kuliko jana na ya jana yawe bora zaidi kuliko ya kesho," alisema MwanaFA na kuongeza kusema kwamba,
"Kura mtakazopiga ni kulipa shukrani na fadhila kwa Mheshimiwa Rais wetu ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa miaka hii minene, hakika Rais ameing'arisha CCM na kutufanya tutembee kifua mbele kutokana na miradi tuliyoitekeleza kwenye ilani yetu ya uchaguzi."
Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga Tedy Makiyao ambaye aliwaeleza wananchi kwamba, sumu haijaribiwi kwa kuonja hivyo, wananchi wa Muheza wanayo sababu ya kuwachagua wagombea wa CCM yenye utaratibu mzuri wa uongozi kuanzia ngazi ya balozi, tawi, kata, wilaya, mkoa na taifa, tofauti na vyama vingine.
Amesema kuwa, hakuna chama ambacho kinaweza kuwaletea maendeleo wananchi kama Chama Cha Mapinduzi ambacho kimejipambanua kuwaletea wananchi maendeleo hivyo, wasifanye makosa.
Amesema vyama vingine vimekuja wakati wa uchaguzi, lakini baada ya kumalizika uchaguzi havitaonekana hata kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao hivyo, wananchi wasipoteze muda kuwachagua.Amerejea kuwaeleza wananchi kwamba, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameleta fedha nyingi nchini kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na madiwani wa kata na viti maalum wa Tarafa ya Bwembera ambao walipopata nafasi waliomba kura na kueleza kwamba, tarafa hiyo haitapoteza kijiji na kitongoji hata kimoja.
No comments