CCM DODOMA MJINI YAWAFIKIA MABALOZI 2,242 KUWAANDAA NA UCHAGUZI NOVEMBA 27, 2024
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini akizungumza na mabalozi wa jimbo lake
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
UONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Dodoma leo umekamilisha kuwafikia mabalozi wote 2,242 wa Jimbo la Dodoma Mjini lenye kata 41 na mitaa 223 kwa kukutana na mabalozi wa Tarafa ya Zuzu kutoka kata za Chigongwe, Nala, Mbalawala, Mbambala, Zuzu, Matumbulu na Mpunguzi.
Mikutano hiyo ni mfululizo wa mikutano inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde. Charles Mamba ya kukutana na mabalozi wote wa Dodoma Mjini kwa lengo la kuwajengea uwezo na kutoa hamasa ya wana CCM kushiriki kwa wingi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Tumezungumza pamoja na kuelewana vizuri na mabalozi wetu, wapo tayari kukamilisha ushindi wa kishindo wa CCM."
"Hili ndiyo jeshi kubwa la CCM tukutane Novemba 27,2024 kwenye uchaguzi ambao naamini CCM itafanya vizuri sana kwa kuwa, tumejipanga na kujiandaa vizuri," alisema Mamba.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini amewapongeza mabalozi kwa kazi nzuri ya hamasha wakati wa kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na kuwaomba kufanya vizuri zaidi kuhamasisha watu wajitokeze na kuichagua CCM.
Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini Sofia Kibaba amewataka mabalozi wote kuzingatia taratibu zote za uchaguzi na kuhakikisha wanaongoza ubalozi wao kupiga kura mapema kabisa.
No comments