Header Ads

ad

Breaking News

Pijei akubalika Kawe, wanne wamfuatia

Mtia nia Jumaa Mhina maarufu Pijei, akinadi sera zake leo.

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wa Jimbo la Kawe Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaama, wameonesha imani kubwa kwa watia nia watano walio kwenye mchakato wa kuomba kuchaguliwa kuwa wabunge wa jimbo lao.

Katika kata zaidi ya tano za jimbo hilo, mtia nia Jumaa Mhina 'Pijei', amekuwa akitajwa na kupendwa hata katika kujieleza wanachama walikuwa wakikubali sera zake zinazotolewa na CCM, huku akifuatiwa na wengine wanne.

Akizungumza na gazeti hili, Juma Abdallah mkazi wa Boko, alisema kuwa, wamefurahishwa na mipango ya Pijei ya kuwaendeleza wakazi wa jimbo hilo, huku akisisitiza wamchague yeye kupeperusha bendera ya chama hicho.

Abdallah alisema mtia nia mwingine mwenye kueleweka ni Colman Masawe, Kippi Warioba, Elias Nawera na John Mayanja ambao wanakaribiana kwa mujibu wa mwanachama huyo.

Mbali na Abdallah, Halima Mwakatobe mkazi wa Kawe Kata ya Makongo, alisema wagombea hao wamejieleza vizuri, lakini watano ndiyo zaidi.

Alisema kuwa, anaamini kama mambo yakienda kama yalivyo bila kuchakachua, Pijei ataweza kupeperusha bendera ya CCM kutokana na mambo aliyoeleza kuwa, atayafanya ikiwa atapa ridhaa ya wana CCM wa jimbo hilo.

Alisema Pijei alizungumzia mambo ya ujasiriamali ambao anaufanya, akiwa ametoa ajira nyingi kwa vijana wa jimbo hilo, lakini mwamuzi wa mwisho ni Agosti Mosi kwenye kapu la kura.

"Kupendwa ama kutopendwa kwa watia nia ni siku ya mwisho ya kura za wanachama, naamini Jimbo la Kawe tutalikomboa wakati huu, lakini akiwekwa mtu anayependwa na wananchi," alisema Mwakatobe.

Mbali na wanachama hao, mwingine Athuman Majimbo, alisema kuwa, maneno mengi yatasikika wakati huu wa kampeni za kuomba kura kwa watia nia wa CCM, lakini sanduku la kura ndilo litakalomaliza kila kitu.

"Unajua chama chetu kina demokrasia pana sana, hivyo tegemea kumpata yule anayetakiwa na wananchi wa Kawe," alisema.

No comments