Header Ads

ad

Breaking News

Rage apigwa 'stop' Simba, kivumbi akirejea safarini

Ismail Aden Rage
Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Simba, imemuengua mwenyeti wao Ismail Rage, na kuvunja benchi zima la ufundi la klabu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo jana, Kaimu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Joseph Itang'are, amesema katika kikao hicho kilichofanyika juzi, kilijadili mambo mbalimbali, likiwemo suala la Mwenyekiti wao, Rage.

Itang'are amesema katika kikao hicho, walijadili suala la kamati ya ufundi, ambayo ilikutana hivi ikiwa imepeleka mapendekezo, ambayo baadaye yalipitiwa na Kamati ya Utendaji na kuyatolea maamuzi.

Amesema maamuzi waliyochukua ni pamoja na kuwaondoa makocha wote wa timu hiyo na kuweka safu mpya, ambayo itakuwa chini ya Kocha Zdravok Logarusic kutoka nchini Croatia, huku msaidizi wake akiwa Selemani Matola.

Itang'are amesema Matola atakuwa kwa muda kwani majukumu yake ni kufundisha timu ya vijana, watamleta mwingine ambaye ataisaidiana na kocha mkuu. Alisema makocha hao wataanza kazi Desemba 2, ambapo kocha huyo atawasili nchini Desemba Mosi. Lakini, kivumbi kitatimka mara atakaporejea nchini.

Itang'are amesema kwa upande wa kocha wa makipa, nafasi hiyo ilikuwa chini ya Kocha James Kisaka, ambaye aliondoka bkwa tatizo la jicho, nafasi yake itatangazwa baada ya kumpata mrithi wake.

Hata hivyo, kwa upande wa Kocha Abdallah 'King' Kibaden na Jamhuri Kihwelu 'Julio', kamati hiyo imesema Julio tayari amemaliza mkataba wake, wakati Kibadeni wamevunja mkataba wake.

Akimzungumzia Rage, amesema Kamati ya Utendaji imefikia uamuzi wa kumsimamisha Mwenyekiti kwa kukiuka taratibu na maadili ya uongozi.

Itang'are amesema hivi karibuni, mwenyekiti huyo ambaye sasa yupo safarini, alimwambia kuwa, ilikuwa uwepo mkutano mkuu wa kupitisha marekebisho ya katiba, ambapo sasa hautafanyika na kuwataka wawaagize matawi yaendelee kupokea maoni ya marekebisho hayo.

Amesema baada ya kupata kauli hiyo, wakaona kama haiwatendei haki katiba yao, kwani tayari walitangaza mkutano mkuu huo wa marekebisho hayo, ambayo ni muhimu kwao kuyafanya.

Itang'are amesema kuwa, hivyo katika kikao hicho kilichokuwa na wajumbe wote wa kamati ya utendaji, waliochaguliwa pamoja majumbe aliyeteuliwa, ambapo kolamu ilitimia waliamua kufanya kikao hicho.

Amesema kuwa, yeye atakaimu nafasi ya Rage, wakati Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swed Mkwabi, atakuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo.

Itang'are amesema kifungu kilichowapa mamlaka hayo ni ibara ya 30M, ambacho kinawapa nafasi wajumbe wa kamati ya utendaji kutoa uamuzi wanaoona unafaa, endapo kuna mjumbe atakuwa ameonesha kwenda tofauti.

Amesema mkutano wa marekebisho ya Katiba utafanyika Desemba Mosi, ambapa suala la Rage litapelekwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu.

"Tumekaa na kuona kuna kila sababu ya kuchukua maamuzi kama haya, tutampeleka kwenye mkutano mkuu ili wajumbe wakatoe maamuzi yao," amesema Itang'are.

No comments