Yanga baba lao mapato Ligi Kuu
![]() |
Yanga wakifurahia moja ya mabao yao. |
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, imedhihirisha kuwa, ina mashabiki wengi wanaopenda kuhudhuria mechi zake, baada ya kufanikiwa kuingiza kitita cha sh. milioni 334.2 kwa kucheza mechi 13 za mzunguko wa kwanza uliomalizika hivi karibuni.
Yanga imevuna kiasi hicho cha fedha na kuwabwaga mahasimu wao, Simba, walioijiingizia sh. milioni 302, wakizidiwa kwa sh. milioni 32.2.Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL), Silas Mwakibinga, alisema mapato hayo ya Yanga ni kwa mechi za nyumbani na ugenini.
Watani wao wa jadi Simba, wameshika nafasi ya pili kwa kujikusanyia sh.milioni 302, katika mechi zake za nyumbani na ugenini, huku timu ngeni katika ligi hiyo iliyopanda daraja msimu huu ya Mbeya City, ikinyapata kitita cha sh. milioni 83.8, katika mzunguko huo na kushika nafasi ya tatu.
Mwakibinga alisema kuwa, Azam FC imechukua nafasi ya nne kimapato kwa kupata kiasi cha sh.milioni 67, wakati Coastal Union ikishika nafasi ya tano kwa kupata sh.milioni 65.7, huku Mtibwa Sugar ikishika nafasi ya sita kwa kupata sh.milioni 49,9 kwa kucheza mechi zake kwenye Uwanja wa Manungu na nje.
Ruvu Shooting imeshika nafasi ya saba ikijinyakulia kitita cha sh. milioni 46.1, wakati Prisons imeingiza sh. milioni 38.1, huku JKT Ruvu ikiweka kibindoni sh.milioni 36.1.
Ashanti United imeshika nafasi ya 10 kwa kubeba kitita cha sh.milioni 35,7, wakati Rhino Rangers ikipata sh.milioni 31.1.
Wakati Mgambo JKT ikishika nafasi ya 12, kwa kujikusanyia sh.milioni 25.8, JKT Oljoro wao walipata sh. milioni 20.8 kwa kushika nafasi ya 13, huku Kagera Sugar ikishika nafasi ya mwisho kwa kuambulia sh.milioni 18.5.
Mwakibinga alisema anaamini katika mzunguko ujao, tiketi za Kieletroniki zitakuwa zimeanza, hivyo mapato ya mzunguko huo yatazinufaisha zaidi timu hizo.
No comments