Yanga mwendo mdundo, yaipiga Polisi Moro 3-0
![]() |
Yanga hao |
Na Mwandishi Wetu
YANGA wameendeleza wimbi la ushindi
katika mechi zao za hivi karibuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuichapa
Polisi Morogoro mabao 3-0, katika mchezo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, leo.
Pamoja na ushindi huo, Yanga
imeendelea kushika nafasi ya tatu katika ligi hiyo kwa kufikisha pointi 17,
ikiwa nyuma ya vinara Simba wenye pointi 19 sawa na Azam wanaoshika nafasi ya
pili kutokana na kuzidiwa idadi ya mabao na Wekundu wa Msimbazi hao.
Yanga walioanza vibaya ligi hiyo kwa
kutoka suluhu na Prisons ya Mbeya ugenini kabla ya kupokea kipigo cha mabao 3-0
ugenini kwa Mtibwa Sugar ya Morogoro, jana walipata bao la kwanza katika dakika
ya tano kupitia kwa Simon Msuva aliyetumia vyema pasi maridadi ya Jerryson
Tegete.
Dakika moja baadaye, mshambuliaji wa
Yanga kutoka Burundi, Didier Kavumbagu, aliipatia Yanga bao la pili baada ya
kuwatoka mabeki wa Polisi Morogoro na kipa wao, Manji Kulwa na kuukwamisha
mpira nyavuni.
Mganda Hamis Kiiza aliyetokea benchi
kuchukua nafasi ya Tegete, aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 56, baada ya
kuunganisha krosi iliyochongwa na David Luhende kutoka wingi ya kushoto.
Msuva nusura aipatie Yanga bao la
nne dakika ya 68, pale alipopata mpira akiwa ndani ya eneo la hatari na kupiga
shuti lililombabatiza kipa wa Polisi Morogoro aliyechukua nafasi ya Kulwa,
Kondo Salum, na kumrudia na kupiga tena fyongo iliyookolewa na kipa huyo kwa
mara nyingine na kuwa kona butu.
Polisi Morogoro walipata nafasi za
kufunga katika dakika za 30, 54, 74 na 87 kupitia kwa washambuliaji wao, Malimi
Busungu, Mokili Rambo na Nicholas Kabipe, lakini walishindwa kuzitumia kupata
mabao kutokana aidha na umakini wa kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ au
kujichanganya kwao.
Kwa ujumla, Yanga waliwazidi Polisi
Morogoro kila idara katika mchezo huo ulioonekana kuwa wa upande mmoja, hasa
katika kipindi cha pili.
Kwa upande wao, Polisi Morogoro
walijitahidi kufurukuta kipindi cha kwanza, lakini katika kipindi cha pili,
timu hiyo ilionekana kusambaratika na kupoteana hivyo kuwapa nafasi Yanga
kujinafasi kadri walivyotaka.
Iwapo washambuliaji wa Yanga
wangekuwa makini zaidi, wangepata mabao mengi zaidi katika mchezo huo, kwani
walikuwa wakipata nafasi lukuki ambazo hata hivyo walishindwa kuzitumia
ipasavyo, ama kutokana na papara au uchoyo wa kupeana pasi wao kwa wao kuelekea
lango la Polisi Morogoro.
Yanga: Ally Mustapher
‘Barthez’, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub
‘Cannavaro, Athuman Idd ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Nurdin Bakari,
Jerry Tegete/Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na David Luhende/Nizar Khalfan.
Polisi Moro: Manji Kulwa/Kondo
Salum, Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Salmin Kisi, Hamisi Mamiwa,
Bantu Admin, Paschal Maige, Mokili Rambo, Malimi Busungu na Nicholas Kabipe/
Keneth Masumbuko.
Kutoka Uwanja wa Azam Complex Chamazi,
Mwandishi Wetu anaripoti kuwa,
mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Azam FC dhidi ya Ruvu Shooting
ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ruvu
Shooting walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Seif Abdallah, lakini
Azam FC walisawazisha kupitia kwa mshambuliaji wao wa kimataifa, Kipre
Tchetche, bao lililozifanya timu hizo kugawana pointi.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza,
Mbeya City imeichapa Burkina Faso bao 1-0, katika mechi iliyochezwa kwenye
Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, jana.
ciao
No comments