Yanga balaa, yaikamata Simba
![]() |
Didier Kavumbagu (kushoto) na Ramadhan Malima wa Mgambo, wakiwania mpira, jana. |
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa soka wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga, jana
imefanikiwa kukifikia kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara na Simba, baada ya
kuicpiga Mgambo JKT mabao 3-0, mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar e Salaam, hivvo kufikisha pointi 23.
Pointi hizo zinaifanya timu hiyo
kulingana na Simba waliotoka sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro kwenye Uwanja
wa Jamhuri, mjini Morogoro jana.
Yanga imefanikiwa kulingana pointi
na Simba, ikiwa ni baada ya mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, kuanza
vbaya ligi hiyo kwa kutoka suluhu na Prisons mjini Mbeya, kabla ya kupokea
kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro.
Mwenendo huo wa kusuasua katika ligi
hiyo, ulionekana kuwakera wapenzi wa timu hiyo na kuanza kukata tama ya timu
yao kufanya vema kwenye ligi hiyo, huku watani wao wa jadi, Simba, wakiwakejeli
kadri walivyotaka.
Lakini hatimaye wapenzi wa timu hiyo
kwa sasa hawana shaka tena na maswali yao juu ya mwenendo wa timu yao, huenda
yamepata majibu, kwamba uwezekano wa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ni mkubwa mno
kutokana na kasi ya ‘chama’ lao hilo, wakiwa wameshinda mechi tano mfululizo.
Katika mchezo huo, Yanga walianza
kuandika bao lao la kwanza katika dakika ya nne kupitia kwa beki wao, Nadir
Haroub ‘Cannavo’, aliyeunganisha krosi ya beki mwenzake, Mbuyu Twite.
Bao hilo lilionekana kuwaamsha
usingini Mgambo JKT ambao walijipanga na kupeleka mashambulizi kadhaa katika
lango la Yanga, lakini safu ya ulinzi ya timu hiyo, ilikuwa imara kuondosha
hatari hizo.
Wakicheza kwa usongo wa kufunga
mabao zaidi, Yanag walipata bao la pili lililofungwa na mshambuliaji wao raia
wa Burundi, Didier Kavumbagu katika dakika ya 41, akiunganisha vema krosi
maridadi ya Mganda Hamis Kiiza ambaye naye alipokea pasi ya beki wa kushoto,
Oscar Joshua.
Akiingia kutokea benchi katika
dakika ya 68, Jerry Tegete, kwa mara nyingine alithibitisha umahiri wake wa
kucheka na nyavu anapokuwa mbele ya lango, baada ya kuifungia Yanga bao la tatu
dakika ya 80.
Baada ya bao hilo, Yanga walihaha
kuongeza bao la nne ambalo lingewawezesha kushika usukani wa ligi hiyo kwa kuwa
na idadi kubwa ya mabao ya kufunga, huku wastani wa mabao ya kufunga na
kufungwa wakilingana na Simba, yaani mabao 12.
Pamoja na kufungwa, Mgambo JKT,
walionesha kandanda ya hali ya juu, wakimiliki mpira na kuonana vilivyo, lakini
walishindwa kufurukuta kwa kuzidiwa uzoefu na wakali hao wa Jangwani.
No comments