TASWA yampongeza Wambura, Mkutano mkuu waiva
![]() |
Katibu Mkuu TASWA |
Na Mwanadishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimepongeza mwanachama wake Boniface
Wambura, kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa
mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za
Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
Katika taarifa
iliyosambazwa leo na chama hicho, kupitia Katibu Mkuu wake, Amir Muhando,
alisema wamepokea kwa furaha uteuzi huo wa Wambura ambaye ni Ofisa Habari wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na inaamini ataendelea kufanya vizuri kama anavyotekeleza majukumu yake ya kazi ndani ya TFF.
“Katika hili waandishi wa
habari za michezo nchini ni mashahidi wa hilo
kwani amekuwa mtu sahihi kwao na amekuwa na ushirikiano mkubwa usio na kifani
kwa wanahabari wenzake.
“Kwa vile Wambura ni
mwanachama wetu hai wa TASWA, kwa kuteuliwa kwake huko ni faraja kwa chama na
tunamtakia kila la heri ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani hiyo ni
ishara tosha kwamba kazi yake inaonekana na inathamanika,” alisema.
Uteuzi wa Wambura,
umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa
fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28
mpaka Novemba 11, mwaka huu.
Wengine walioteuliwa ni
ofisa kutoka Makao Makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.
… Mkutano mkuu wanukia
Na Mwandishi Wetu
SSKRETARIETI ya Chama cha
Waaandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA), imefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini wa Mkutano Mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao katika tarehe ambayo itatangazwa rasmi.
Kamati ya Utendaji ya
TASWA, ilikubaliana katika kikao chake mwezi uliopita kuwa Mkutano Mkuu wa
TASWA mwaka huu uwe wa aina yake kwa kuwawezesha wanachama kukaa pamoja na
kubadilishana mawazo na ikashauri ikiwezekana ufanyike nje ya Dar
es Salaam kama hali itaruhusu.
Kutokana na hali hiyo,
kikao kiliiagiza sekretarieti ya TASWA itafute mdhamini wa kufanikisha suala hilo na kwamba kama ikishindikana mkoani ifanyike Dar es Salaam lakini kuwe
na mdhamini.
“Tayari hilo limefanyika na mdhamini amepatikana,
ambapo hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini itakuwa mapema wiki
ijayo na baada ya hapo itatangazwa tarehe rasmi.
“Nichukue nafasi hii
kuwaomba wanachama ambao hawajalipa ada zao wafanye hivyo kwa kuwasiliana na
Mhazini wa chama au Mhazini Msaidizi ili waepuke usumbufu wa kushindwa
kuhudhuria mkutano huo,” alisema Mhando.
No comments