Header Ads

ad

Breaking News

Okwi namba nyingine Simba, aonesha kiwango


Okwi

*Azam FC yapigwa 3-1, kama wamelala

Na Mwandishi Wetu

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wamezidi kujikita kileleni mwa ligi hiyo baada ya leo, kuikandamiza Azam mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku nyota wake, Emmanuel Okwi, Shomary Kapombe, Felix Sunzu na Mrisho Ngassa waking’ara vilivyo.

Kwa matokeo hayo, Simba wamefikisha pointi 22, huku Azam wakibakiwa na pointi zao 18 na hivyo kuporomoka hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya Yanga kuichapa JKT Oljoro bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kuipoka Azam nafasi ya pili.

Katika mchezo huo wa jana, Azam ndio walioanza kupata bao lililofungwa na John Bocco katika dakika ya nne baada ya kupokea pasi ya Salum Abubakari na kuwafungasha mabeki wa Simba, Paschal Ochieng na Shomari Kapombe kutoka katikati ya uwanja na kumchambua vilivyo kipa wa Simba, Juma Kaseja kuipa timu yake bao la kwanza.

Bao hilo liliwazindua Simba na kujipanga kufanya mashambulizi ya nguvu na hatimaye kusawazisha dakika tatu baadaye kupitia Mzambia Felix Sunzu aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Said Nassor ‘Chollo’.

Katika dakika ya 40, Emmanuel Okwi aliifungia Simba bao la pili kwa kichwa, akiunganisha vema krosi ya kiungo Mwinyi Kazimoto kutoka wingi ya kushoto.

Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 51, akipiga kiufundi mno mpira uliotinga moja kwa moja nyavuni akiwa nje kidogo ya 18.

Baada ya mabao hayo, Simba walionekana kucharuka zaidi na kuichezesha mchakamchaka Azam kadri walivyotaka, ambapo Okwi, Ngassa, Sunzu na beki Shomari Kapombe waling’ara mno.

Dakika ya 17, Kazimoto alipiga shuti kali akiwa nje kidogo ya 18, lakini shuti hilo lilitoka nje kidogo ya lango la Azam.

Hamis Mcha aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Bocco aliyeumia, aliikosesha Azam bao baada ya kushindwa kutulia akiwa ndani ya sita ya lango la Simba ambapo alipiga fyongo iliyookolewa na Kaseja.

Iwapo mchezaji huyo angekuwa makini, angempasia Kipre Tchetche aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini alilazimisha kufunga akiwa katika pembe ya goli na kushindwa kufanya hivyo.

Okwi nusura afunge bao katika dakika ya 35 ambapo shuti lake akiwa pembeni ya lango la Azam, liligonga mwamba na mpira kumkuta Mrisho Ngassa aliyepiga shuti kali lililowababatiza mabeki wa wapinzani wao hao.

Kazimoto alikosa bao la wazi katika dakika ya 46 akiwa ndani ya 18 ambapo shuti lake lililotokana na pasi maridadi ya Okwi, lilidakwa na kipa wa Azam, Mwadini Ally.

Dakika ya 79, Ochieng aliokoa bao la wazi la Azam kutokana na mpira wa kichwa uliopigwa na Kipre na kuokolewa na beki huyo katika mstari wa goli.

Simba: Juma Kaseja, Said Nassor ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Paschal Ochieng, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba/Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Felix Sunzu/Ramadhan Singano ‘Messi’, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Christopher Edward.

Azam: Mwadini Ally, Ibrahim Shikanda, Sahm Nuru, Said Morad, Agrey Morris, Addulhalim Humoud, Jabir Aziz/Bolou Michael, Himid Mao/Abdu Kassim ‘Babi’, John Bocco/Hamis Mcha, Kipre Tchetche na Salum Abubakar.

No comments