Mashabiki Yanga, Simba waichangia Innovate 200,000
Mkurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Innovate, George Ndaki
Na Omary Mngindo, Kibaha
WANACHAMA na mashabiki wa klabu za Yanga na Simba Mlandizi na viunga vyake, wameichangia Shule ya Awali na Msingi ya Innovate kiasi cha Shilingi 200,000.
Wamefanikisha hilo kupitia hamasa ya nani zaidi katika kuchangia elimu, kwenye mahafali ya pili shuleni hapo iliyopo Kitongoji cha Kibwende Kata ya Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, chini ya mshereheshaji Jackline Edward.
Mbele ya mgeni rasmi, Revina Lemomo, Mdhibiti Mkuu Ubora wa shule wilayani hapa akimwakilisha mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa, alisema kuwa wanapenda kuunga mkono juhudi za Mkurugenzi wa shule hiyo, George Ndaki.
"DJ niletee wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu za Yanga na Simba tuone klabu ipi inajitoa katika kuchangia katika uendelezaji wa elimu shuleni hapa, tuanze na Simba weka wimbo wao tuwaone uwanjani," alisema Jackline.
Baada ya DJ kuweka muziki uliozungumzia klabu hiyo, wana Simba wakajitosa uwanjani huku kila mmoja akijipapasa mfukoni na katika pochi wakitoa walichonacho, kabla ya kuwainua wana Yanga, ambao vivyo hivyo wakachanga kama ilivyo kwa wana Simba.
Awamu ya kwanza ilipoisha wana Simba walipata zaidi ya Shilingi 30,000, wakati Yanga wakiwazidi kwa kukusanya zaidi ya Shilingi 60,000, hali hiyo ilipingwa na wana Simba kwa kukata rufaa hivyo, kuomba kurudiwa kwa zoezi hilo.
Mpaka mwisho wa ushindani huo wakajikuta kila klabu ikichangia kiasi cha Shilingi 100,000 hivyo, kuwezesha kupatikana kwa Shilingi laki mbili.
Akizungumza baada ya kushindanishwa, Mkurugenzi Ndaki aliwashukuru wanamichezo hao kwa kujitoa huko, na kwamba kiasi hicho watakitumia kwenye ujenzi unaonedelea shuleni hapo.
"Nawashukuru sana wazazi, walezi na wote mnaoendelea kuitakia mema shule yetu, nasi katika sekta hiyo kama mnavyoona tuna viwanja vya michezo mbalimbali, tunawaahidi tutaendeleza vijana katika elimu na michezo," alimalizia Ndaki.


No comments