Dkt.Mwinyi asema Serikali imeweka mfumo madhubuti ufuatiliaji miradi
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali imeweka mfumo madhubuti wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi itakayotekelezwa kupitia fedha za Zanzibar Sukuk.
Alieleza hayo alipoifunga Awamu ya Kwanza ya Uwekezaji wa Hatifungani ya Zanzibar Sukuk Hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu , Zanzibar.
Dkt. Mwinyi alisema fedha zilizopatikana zitapelekwa moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo yenye tija ikiwemo miradi ya miundombinu ya barabara za Unguja na Pemba, bandari jumuishi ya Mangapwani, Kituo cha Matibabu ya Saratani cha Binguni na kumalizia kazi ya ujenzi wa jengo la abiria la Terminal 2 la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Alieleza kuwa,mafanikio yaliyopatikana katika Awamu ya Kwanza ya Zanzibar Sukuk yameifanya Zanzibar kuwa kituo cha kujifunzia kwa cchi za Afrika Mashariki na baadhi ya nchi za katika uendeshaji wa mpango huo.
Dkt.Mwinyi alieleza kuwa, mafanikio hayo yameonesha dhamira thabiti ya serikali ya kuwa na uchumi jumuishi unaowashirikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza.
Aidha, alisema kuwa kwa mafanikio hayo hivi karibuni serikali inakusudia kuanzisha Soko la Mitaji la Zanzibar yaani Zanzibar Securities Exchanges, ambalo litasaidia kupatipakana kwa mitaji ya kuwekeza katika biashara mbalimbali pamoja na miradi mikubwa ya serikali hatua aliyoielezea kuwa ni muhimu kufikia lengo la nchi kuwa ni Kituo cha Fedha (Financial Hub).
Rais ameipongeza Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais Fedha na Mipango na Taasisi ya Ufuatiliaji wa Mipango ya Serikali (PDB) kwa kufanikisha mpango huo, kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu zaidi kuibua njia mbadala za kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Amewapongeza wawekezaji wote waliowekeza katika awamu hiyo ya kwanza na kuwasisitiza kufanya hivyo katika awamu nyingine ili kuunga mkono juhudi za serikali.
Amewahakikishia wawekezaji hao kuwa, mapato ya kila mwaka ya asilimia 10.5 na yale ya asilimia 4. 2 kwa wanaowekeza kwa dola pamoja na fedha za mitaji zilizowekezwa kila baada ya miaka aba yatapatikana kwa wakati kama ilivyoainishwa katika masharti ya mpango huo.
Rais Dkt.Mwinyi amewasisitiza wananchi kudumisha amani na mshikamano kwani bila ya kuwepo amani hakuna mafanikio ya aina hiyo yanayoweza kupatikana.
Naye, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha na Mipango Saada Mkuya Salum amesema zaidi ya shilingi bilioni 381, sawa na asilimia 128.33 zimewekezwa katika awamu ya kwanza ya Zanzibar Sukuk na kuvuka makadirio ya awali ya shilingi bilioni 300.
No comments