Mahujaji zaidi ya 1.7 milioni kutoka nchi mbalimbali wamesafiri kwenda Mecca kwa Hajj. (AFP)
Mahujaji karibu
milioni mbili kutoka nchi mbalimbali duniani wameanza kuwasili Saudi
Arabia kwa ibada ya Hajj ambayo hufanyika kila mwaka.
Walianza machweo Jumatano kwa kuzunguka Kaaba katika Msikiti Mkuu wa Mecca, eneo takatifu zaidi katika dini ya Kiislamu.
Raia wa Iran kwa mara nyingine wanashiriki baada ya kukosa Hajj ya mwaka mmoja kutokana na mkanyagano uliotokea mwaka 2015.
Kulikuwa
na taarifa za kukinzana kuhusu idadi kamili ya mahujaji wanaohudhuria
kutoka taifa jirani la Qatar, ambalo limekuwa kwenye mzozo mkali na
Saudi Arabia.
Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu, ambayo
inafadhiliwa na serikali ya Qatar, imesema ni raia wachache sana wa
Qatar ambao wamevuka mpaka, ambao ulifunguliwa wiki mbili zilizopita na
serikali ya Saudia kuwawezesha Waislamu kuhiji.
Lakini
gavana wa Mecca amesema raia 1,564 wa Qatar wanashiriki ibada hiyo ya
Hajj, idadi ambayo imeongezeka ukilinganisha na 1,210 mwaka jana.
Kwa Waislamu, Hajj ndiyo nguzo ya tano na ya mwisho ya dini ya Kiislamu.
Ni
ibada ambayo Mwislamu yeyote aliyekomaa anashauriwa kutimiza angalau
mara moja maishani mwake iwapo anaweza kulipia gharama na ana nguvu za
kimwili kuweza kutimiza abada hiyo. Serikali ya Saudia imesema imechukua tahadhari kuzuia kutokea tena kwa mkanyagano sawa na uliotokea miaka miwili iliyopita.
Maafisa
wa Saudia wanasema mahujaji karibu 800 walifariki wakati wa mkanyagano
huo, lakini takwimu zisizo rasmi zinasema watu zaidi ya 2,400
walifariki.
Iran pekee ilikuwa na raia 464 waliofariki na baada ya
hapo iliwatuhumu maafisa wa Saudia ikisema wanafaa kulaumiwa kwa vifo
vilivyotokea.
Maafisa wa Saudia walikanusha tuhuma hizo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani wa Saudia Meja Jenerali
Mansour al-Turki amesema maafisa wa usalama zaidi ya 100,000 wametumwa
katika maeneo mbalimbali ya Mecca na Medina kulinda na kuwaelekeza
mahujaji.
Aidha, kuna kamera nyingi sana za usalama.
Waislamu milioni mbili waanza ibada ya Hajj Mecca
Reviewed by Majuto Omary na Frank Balile
on
3:32 PM
Rating: 5
No comments