WAFANYAKAZI WA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) WATAKIWA KUFANYA KAZI ZAO KWA UFANISI
![]() |
Profesa Mohamed Janabi |
Wafanyakazi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma,
kuongeza ufanisi na kutoa huduma bora kwa wagonjwa ili
epukana na malalamiko yanayoweza kujitokeza.
Rai hiyo imetolewa leo
na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza
katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Prof. Janabi pia
aliwahimiza wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuendelea kutunza vizuri
kumbukumbu mbalimbali zikiwemo za wagonjwa na utendaji wa kazi zao za kila siku
ili pale zitakapohitajika zipatikane kwa haraka.
“Mjitahidi kujaza fomu
ya wazi ya mapitio na upimaji utendaji kazi (OPRAS) kwa wakati ili kusiwe na
malalamiko ya upandaji wa vyeo kwani ujazaji wa fomu hizo ndiyo unaowezesha
mfanyakazi kupimwa utendaji wake kwa kipindi cha mwaka mzima”, alihimiza
Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Godfrey
Tamba aliupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha
wafanyakazi wanafanya kazi zao katika mazingira bora.
Tamba alisisitiza,
“Wafanyakazi wenzangu tunaodai haki zetu tukumbuke kutimiza wajibu wetu wa kazi
kwa wakati, kwani uongozi wa TUGHE hautawatetea watu ambao hawatimizi wajibu
wao ipasavyo”.
Hiki ni kikao cha pili
cha wafanyakazi wote kufanyika tangu kuanza kwa mwaka huu ambapo katika kikao
hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika
utendaji wa kazi.
No comments