Cheka akata rufaa BMT kupinga matokeo
Na Mwandishi Wetu
BONDIA wa ngumi za kulipwa
nchini, Cosmas Cheka amekata rufaa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kupinga
matokeo na adhabu ya kufungiwa miezi sita na faini ya Sh200,000 iliyotangazwa
na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC).
Cheka amesema hayo leo kwenye
mkutano na waandishi wa habari na kusema kuwa TPBC ilikuwa na njama dhidi yake
ili kumtengenezea nafasi bondia Haidary Mchanjo katika ngumi za kulipwa nchini.
Amefafanua kuwa adhabu dhidi yake
haikufuata sheria kwani kwanza hakupewa nafasi ya kusikilizwa kwa mujibu wa
sheria, huku akimpa nafasi mwamuzi wa pambano hilo, Modest Rashid ambaye
alitaka kupigana naye kuitwa na kujieleza katika kikao cha TPBC.
“Hata kwenye mahakama, lazima
mtuhumiwa apewe nafasi ya kusikilizwa au kujitetea, mimi nilikuwa ulingoni na
mwamuzi na mpinzani wangu Mchanjo, mwamuzi amenitolea maneno machafu sana,
haikutosha akaamua kunikata pointi, niliandika barua ya kulalamika TPBC,
hawajaniita na kuibuka na adhabu kwangu,” amesema Cheka.
Amesema kuwa pamoja na maamuzi hayo
kutonifikia kimaandishi, nimeamua kuchukua hatua za haraka kwani tayari vyombo
vya habari mbalimbali na mitandaa ya kijamii yamekwisha tangaza maamuzi hayo
yaliyofanywa bila kufuata sheria kwani hawakunipa nafasi ya kusikilizwa kwa
mujibu wa sheria.
Meneja wa bondia huyo, Juma
Ndambile, alisema kuwa walichokifanya TPBC ni kumvunja nguvu bondia wake ili
ashindwe kuendelea na mchezo wake.
Ndambile amesema kuwa TPBC
ilionyesha nia ya kuhujumu matokeo hayo mapema kwa kuweka vipingamizi
mbalimbali pamoja na kutakiwa kumlipa mwamuzi wa pambano wakati wao
hawakuwa waandaaji.
“Nimewaambia kuwa pambano
limeandaliwa na kampuni inayoiitwa dragon, sasa kwa nini mimi nilipe, pia
niliambiwa nitafute hela ya glovu, niligoma, nadhani hiyo ndiyo imekuwa
chanzo,” amesema Ndambile.
Amesema kuwa ili kumpata mshindi
sahihi, bora pambano hilo lilirudiwe ili mshindi apatikane kwa mujibu wa
taratibu na siyo kwa njia iliyotumika ambayo lengo lake ni kuharibu rekodi na
kutengenza za bondia mwigine.
No comments