Waziri Mwakyembe atengua uteuzi wa mwenyekiti BMT
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Harrison Mwakyembe ametengua uteuzi wa mwenyekiti na wajumbe wa Baraza
la Michezo la Taifa (BMT), baada ya kushindwa kupata ufumbuzi wa migogoro katika
michezo nchini.
Maamuzi hayo yametolewa baada ya Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, hivi karibuni kumwagiza Waziri wa Michezo kulipitia baraza hilo na iwapo hataridhika na
utendaji wake, alivunje.
Leo, Waziri Mwakyembe amesema sekta
ya michezo imekuwa na migogoro mingi inayochangia kushusha maendeleo ya michezo
nchini. Mwenyekiti wa BMT alikuwa Dioniz Malinzi.
Amesema agizo hilo la Waziri Mkuu
limekuja wakati sahihi, kwani alifanya kikao na BMT kulielimisha kuhusu wajibu
wake kisheria, changamoto zinazolikabili baraza hilo na hali ya uhuru
uliopitiliza katika uongozi wa uendeshaji wa michezo nchini.
Amesema pamoja na BMT kulalamikia ukosefu
wa fedha kama kikwazo kikubwa kinachokwamisha utendaji kazi wake, wizara imeona
zaidi hitaji la utashi, dhamira na kujituma kuliko fedha katika kutatua sehemu
kubwa ya udhaifu unaotawala tasnia ya michezo.
Waziri Mwakyembe amezungumzia kasoro ya
viongozi wa michezo kushika zaidi ya nafasi moja ya uongozi, vitu
vinavyochangia kushusha kiwango cha michezo nchini, hata ushiriki wa michezo wa
Tanzania nje ya nchi bila kulishikirisha baraza hilo.
Pia, amezungumzia mapromota wa mchezo
wa ngumi kuendesha shughuli zao bila kusajiliwa, chaguzi za vyama vya michezo
kugubikwa na ubabe na rushwa, katiba na kanuni za vyama kutohakikiwa kubaini
upungufu kuhusu masuala ya fedha, tuhuma za rushwa, ubadhirifu, upendeleo na
maamuzi ya kibabe.
Mambo hayo yamemfanya Waziri
Mwakyembe kusema kuwa, baraza litafanya kazi kwa kushirikiana na wizara wakati
taratibu za kumpata mwenyekiti na wajumbe wapya zikiendelea kufanyika kwa
mujibu wa sheria.
No comments