Kili yaipongeza Simba SC kwa mwanzo mzuri
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, akisalimiana na beki wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' wachezaji wa Simba kabla ya mechi yao na Sports Club Villa ya Uganda iliyochezwa mwishoni mwa wiki. Simba ilishinda 1-0.
Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager, imeipongeza Klabu ya Simba kwa mwanzo mzuri baada ya kuifunga Sports Club Villa ya Uganda 1-0, katika mechi iliyochezwa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Pongezi hizo zilitolewa na Meneja wa Kilimanajro Premium Lager, Pamela Kikuli, ambaye alikuwa uwanjani kushuhudi mechi hiyo na kufurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wa Simba ambao walionesha matumaini makubwa mno.
“Sisi kama wadhamini tumefurahishwa mno na ushindi huu kwani unapowekeza sehemu unategemea kupata faida na faida yake ndiyo ushindi kama huu…ni matumaini yetu kuwa, Simba itaendelea kufanya vizuri na kushiriki katika mashindano ya kimataifa,” alisema.
Alisema lazima Simba ianze na matokeo mazuri ya ligi ya ndani ili iweze kupata nafasi ya kucheza nje kama wahasimu wao Yanga.
“Tungependa kuona Simba na Yanga zote zinashiriki katika mashindano ya kimataifa kwani klabu zote hizo zinadhaminiwa na Kilimanajro Premium Lager na zina mashabiki wengi ambao kwa upande mwingine, wanatuunga mkono kwa kuwekeza katika mpira,” alisema na kuongeza kuwa, lengo lao kama wadhamini ni kuhakikisha mpira wa Tanzania unafika katika kilele cha mafanikio.
Aliipongeza Simba pia kwa kusajili vizuri safari hii na pia kumwajiri kocha mzuri ambaye ameielewa timu kwa muda mfupi na kuwapa viongozi wa Simba na wao kama wadhamini matumaini makubwa ya kufanya vizuri zaidi.
“Nilikuwepo uwanjani na nikashuhudi mechi kati ya viongozi wa Simba na mastaa wa Bongo, ambapo viongozi wa Simba walishinda 1-0 na bao hilo la pekee lilifungwa na kocha huyu kutoka Uingereza…hii inaonesha kuwa, ni mtu mwenye uzoefu na atakuwa chachu ya mafanikio katika klabu hii,” alisema Pamela.
Aliwapongeza pia viongozi wa Simba kwa kuiandaa Wiki ya Simba, ambapo walifanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea kiwanda cha Bia Tanzania (TBL). Kwa mujibu wa meneja huyo, shughuli kama hizi za wiki nzima zimesaidia kuitangaza klabu na pia kuwakutanisha wachezaji na mashabiki mbalimbali.
No comments