Lowassa ahamia rasmi Chadema, aeleza sababu za kuihama CCM

Edward Lowassa akiwapungia mkono makada wa vyama vya Ukawa na Chadema baada ya kuwasili ukumbini.

Mwenyekiti wa Chadema , Freeman Mbowe (kushoto) akiteta jambo na Edward Lowassa aliyejiunga na chama hicho leo.

Edward Lowassa (kushoto),akizungumza na Prof. Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF na mwenyekiti mwenza wa Ukawa.

Edward Lowassa akitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema na kuungwa mkono na Ukawa.

Freeman Mbowe (kushoto) akimkabidhi kadi ya Chadema , Edward Lowassa

Lowassa, na mkewe pamoja na meza kuu wakionesha kadi za Chadema A.

Meza kuu ya mkutano huo ikifurahiya jambo.

Baadhi
ya viongozi na makada wa vyama vinavyounda Ukawa na viongozi wa Chadema
wakiwa katika mkutano wa kumtambulisha Edward Lowassa kujiunga na chama
hicho.

Baadhi
ya viongozi na makada wa vyama vinavyounda Ukawa na viongozi wa Chadema
wakiwa katika mkutano wa kumtambulisha Edward Lowassa kujiunga na chama
hicho.
ALIYEKUWA Waziri Mkuu mstaafu wa
Tanzania, Edward Ngoyai Lowassa na kada mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ametangaza rasmi kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) huku akiacha historia ya pekee nchini
Tanzania.
Lowassa ametangaza uamuzi huo leo
alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari, baadhi ya
viongozi wa Chadema na viongozi wakuu wa Umoja wa Katiba ya Watanzania
(Ukawa) katika Hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach Hoteli iliyopo
eneo la Kunduji jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo uliokuwa na
ulinzi mkali kiusalama ambapo kila aliyeingia kwanza alipekuliwa na
kisha kuhakikisha jina lake lilitumwa mapema kwamba anaalikwa kushiriki
mkutano huo na si vinginevyo na watu ambao hawakutambulika wala kualikwa
katika mkutano huo hawakuruhusiwa kuingia ukumbini. Ndani ya ukumbi pia
hakukuwa na ruhusa kusimama zaidi ya waandishi wa habari wapiga picha
ambao waliruhusiwa kutokana na kazi yao.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa
pia na viongozi wa juu wa vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi, NLD pamoja na
wenyeji CHADEMA viongozi wa vyama hivyo ambao ndio wanaounda ushirikiano
wa UKAWA walionekana kumuunga mkono Lowassa wazi wazi kugombea nafasi
ya urais kupitia UKAWA kwa mgongo wa chama cha Chadema. Hata hivyo
hawakutamka moja kwa moja kwamba tayari wameridhia Lowassa kusimama
katika kinyang’anyiro cha urais kwa mwamvuli wa UKAWA.
Akizungumza Lowassa alisema azma
yake ya kusimama kama mgombea urais wa Tanzania ili aweze kuanza
mchakamchaka wa maendeleo ya nchi na kuondokana na umasikini upo pale
pale licha na jina lake kukatwa kinyemela na Chama Cha Mapinduzi Dodoma.
Alisema mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM uligubikwa na
mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa katiba na taratibu za
uchaguzi wa CCM, huku ukiwa na upendeleo mkubwa na kuonesha chuki dhidi
yake.
Alisema kikatiba ya CCM kamati ya
maadili iliyokata jina lake na majina mengine haina madaraka ya kuchuja
na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi lakini ilifanya hivyo. “…Kikatiba kamati ya
maadili ya CCM si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na
kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea Urais kupitia
CCM. Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka
Katiba ya CCM,” Aidha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na
kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia,
Katiba, Kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM,” alisema Lowassa.
Aliongeza kuwa aliwekewa mizengwe
na kuzushiwa majungu na uongo mwingi kuhakikisha jina lake halifikishwi
ndani ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu na kujadiliwa licha ya kuwa
ndiyo mgombea pekee aliyekuwa akiungwa mkono na wanachama na wananchi
ukilinganisha na wenzake wote.
Alisema njama ndani ya CCM dhidi
ya mpango wa kuchafua jina lake si jambo jipya kwani imekuwepo mikakati
hiyo ambayo baadhi ya vijana walitumika kulichafua jina lake na kuzusha
uwongo ambao baadaye walizawadiwa madaraka makubwa.
“…Naamini sikutendewa haki katika
mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteuwa mgombea wa Urais wa
CCM. Nilinyimwa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa kwa
mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nikiendelea kujidanganya mimi mwenyewe
na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa nina imani na CCM au kuwa CCM ni
chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na
kijamii. CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na
kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya
haki, usawa na uadilifu,” alisema na kuendelea…
“..Nidhahiri kwamba CCM imepotoka
na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi
kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema IMETOSHA na SASA
BASI! Kama baba wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere alivyosema,
CCM siyo baba yangu wala mamayangu na Kwamba kama Watanzania hawapati
mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute
mabadiliko nje ya CCM,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na baadhi ya
viongozi wa CHADEMA.
Alisema ameitikiwa wito wa UKAWA
na kuingia CHADEMA ili kushirikiana na umoja huwo kuleta mabadiliko ya
kweli ya taifa, uamuzi ambao ameufanya baada ya kufikiria vya kutosha na
kujiridhisha kuwa ndani ya UKAWA wanaweza kushinda Uchaguzi Mkuu hapo
Oktoba 2015 na kuleta babadiliko hayo ya kihistoria. Aliwaomba
Watanzania wenye nia ya kweli ya kuleta maendeleo na demokrasia ya dhati
kujiunga na umoja huo ili kushirikiana katika safari mpya ya kuinusuru
nchi.
Uamuzi wa Lowassa kuihama CCM na
kujiunga na upinzani ni historia ya kwanza kwa kiongozi aliyeshika
nyazifa za juu za nchi ya Tanzania huku akiwa na ushawishi mkubwa wa
Watanzania kujiunga na upinzani akiwa na mtazamo wa kuleta mabadiliko
ambayo anaamini hayapatikani ndani ya chama hicho. Edward Lowassa
aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu, Waziri na kushika nafasi anuai, kada
mkubwa ndani ya CCM anakuwa ni kiongozi anayeacha historia kwa uamuzi
wake.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments