Azam kuivaa Gor Mahia fainali
Wachezaji wa Azam FC wakishangilia baada ya kupata bao pekee katika mchezo wa nusu fainali ya Kageme dhidi ya KCCA ya Uganda, leo. Azam imetinga fainali ya michuano hiyo. |
Azam FM imeweka historia ya kutinga fainali ya mashindano ya Kagame mara mbili katika kipindi cha miaka mitatu, baada ya kuifunga KCCA bao 1-0, katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mara ya kwanza, Azam FC ilitinga fainali ya mashindano hayo mwaka 2012, ilifungwa Yanga ambao ni mabingwa mara tano wa mashindano hayo, mwaka jana iliishia hatua ya robo fainali.
Bao pekee la Azam FC lilifungwa dakika 90, na kinda kutoka chuo chake cha michezo, Farid Mussa (18), dakika 14, kabla ya filimbi ya mwisho kupulizwa.
Mussa alifunga bao hilo kwa kuunganisha mpira wa krosi uliotoka kwa Ame Ally ‘Zungu’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya.
Farid alirekebisha makosa yaliyofanywa na washambuliaji wa timu hiyo, John Bocco, Kipre Tchetche na Didier Kavumbangu waliopoteza nafasi kadhaa.
Kwa ushindi huo, Azam FC ambao ni timu pekee nchini iliyobaki katika mashindano hayo, baada ya kutolewa kwa KMKM na Yanga, itavaana na Gor Mahia ya Kenya ambayo iliifunga Al Khartoum ya Sudan mabao 3-1, katika hatua ya nusu fainali ya kwanza iliyotangulia.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza katika ya michuano hiyo, huku Gor Mahia ikiwa na rekodi ya kutwaa taji hilo mara tano sawa na Yanga, huku Simba wakiwa wakitwaa mara sita.
Khartoum N na KCC zitamsaka mshindi wa tatu Jumapili, kabla ya mchezo wa fainali.
Bingwa wa mashindano hayo, mbali ya kupata Kombe na medali za dhahabu, atazawadiwa dola 30,000 (ambazo ni takribani sh. milioni 60), mshindi wa pili dola 20,000 (takribani sh. milioni 40), na dola 10,000 (sh. milioni 20), ambazo zitatotolewa na mdhamini wa mashindano hayo Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
No comments