Musley Al Rawahi apania kufanya mambo makubwa Simba Sports Club
Musley Al Rawahi
Na Mwandishi wetu
Mjumbe mpya wa kamati ya utendaji wa
klabu ya Simba, Musley Al Rawahi, amesema kuwa silaha kubwa ya kufikia
maendeleo katika klabu hiyo ni umoja na kufanya kazi kwa kujituma na uadilifu
mkubwa.
Musley ambaye mwaka jana alimzawadia
gari kiungo wa Simba SC, Ramadhani “Messi” Singano kwa kucheza vizuri katika
ligi kuu ya Tanzania Bara, alisema hayo
mara baada ya kutangazwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo na pia
kuwa miongozi mwa wajumbe wanaounda kamati ngumu na nyeti ya usajili wa klabu
hiyo.
Alisema kuwa anashukuru kuteuliwa kuwa
mjumbe wa kamati ya utendaji na usajili wa klabu hiyo na anaamini uteuzi wake
umetokana na jinsi alivyokuwa mstari wa mbele kutafuta maendeleo ya klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Musley, Rais wa klabu
hiyo, Evans Aveva hajafanya makosa katika uteuzi wa wajumbe wa kamati ya
utendaji, usajili, mashindano na soka la vijana kwani hizo ndizo nguzo za
ustawi wa klabu na kufanikisha mambo mengi ya maendeleo.
“Tukisajili wachezaji wazuri, ndiyo
watatuletea ushindi ndani ya klabu na hivyo kamati ya mashindano kufanyakazi
zake kwa ufanisi mkubwa, hivyo natoa wito kwa wajumbe wateule, tufanye kazi kwa
bidii na kuleta maendeleo makubwa klabuni na kuendelea kumpa sifa waliotuteua
kushika nadhifa hizo,” alisema Musley.
Alisema kuwa yeye ana historia kubwa
sana katika klabu hiyo na amekuwa mwanachama tangu akiwa mdogo na hiyo
ilitokana na mapenzi makubwa ya baba yake kwa Simba.
“Mzee wangu amekuwa mwanachama wa klabu
hii kwa miaka mingi, mimi nimefuata nyayo zake na mpaka sasa nimekuwa na klabu
hii kwa miaka mingi, nina uchungu nayo sana, ninaahidi kufanya kazi kwa bidii
ili kufikia lengo,” alisema Musley.
Alisema kuwa changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo ni matarajio ya wanachama na mashabiki wa Simba kwani
wanachotaka wao ni ushindi na kutwaa ubingwa.
“Wana-Simba wanataka ubingwa, hakuna
kingine ambacho wanakitaka, tunahitaji kusajili wachezaji wazuri, wenye kuleta
ufanisi na kutufikisha kule tunakotaka,” alisema.
No comments