Yanga, Prisons suluhu
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
YANGA ya Dar es Salaam, jana iliwabana na Prisons,
na kufanikiwa kutoka suluhu , katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la
Kagame), waliondoka jijini Dar es Salaam wakiamini kuwa, watakwenda kuzoa
pointi zote tatu katika mchezo huo dhidi ya Prisons iliyopanda daraja msimu
huu.
Yanga wanaodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Lager
inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), walianza mchezo kwa kulifikia
lango la Prisons, lakini Said Bahanunzi, dakika ya 19, alishindwa kuuwahi mpira
krosi uliopigwa na Haruna Niyonzima na kuokolewa na beki mmoja.
Pamoja na mashabiki wa Prisons kusimama nyuma ya
goli la Yanga, huku wakishangilia kumchanganya kipa Ally Mustapha ‘Barthez’,
lakini alikuwa makini kuhakikisha nyavu zake hazitikiswi.
Kipindi cha pili Yanga walizidisha mashambulizi,
ambapo dakika ya 64, Simon Msuva, alishindwa kuipatia timu yake bao baada ya
shuti lake kupanguliwa na kipa wa Prisons Dany Abdallah na kuwa kona, ambayo
haikuzaa matunda.
Yanga wakizidi kuliandaa lango mla Prisons, walipata
nafasi nyingine nzuri, baada ya Haruna Niyonzima kutoa pasi nzuri kwa Hamis
Kiiza, lakini shuti lake lilipaa juu kidogo la lango la wapinzani wao.
Prisons ilijibu mashambulizi hayo dakika ya 81,
baada ya Fred Chudu kufanikiwa kuitoka ngome ya Yanga na kupiga shuti kali
lililopanguliwa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Prisons:
Dany Abdallah, Henry Mwalugala, Laurian
Mpalile, Lugano Mwangama, David Mwantika, Khalid Fupi, Sino Augustino,
Fred Chudu, Elias Maguli, Peter Michael, Ramadhan Katamba.
Yanga:
Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdula,
Pscar Joshua/Athuman Idd ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani,
Mbuyu Twite, Nizar Khalfan/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanunzi,
Didier Kavumbagu/Hamis Kiiza, Stephano Mwasyika.
No comments