Azam safi, Mtibwa sare
AZAM FC, baada ya kuikosa Ngao ya Hisani kwa
kufungwa na Simba mabao 3-2, Jumanne iliyopita, jana ilisawazisha mabao yake na
kufanikiwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0.
Katika mechi hiyo ya ligi kuu Bara inayodhaminiwa na
Kampuni ya Simu ya Vodacom, Azam walikuwa ugenini kwenye Uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba, ambapo walifanikiwa kuwanyamazisha mashabiki wa timu hiyo
waliokuwa wakiishangilia.
Bao pekee la Azam lilifungwa na Abdulhalim Humoud,
na kuzima kabisa kelele za mashabiki wa Kagera Sugar waliokuwa wamejaa
uwanjani.
Katika mchezo huo, Humoud alionesha kiwango kizuri
cha soka, ambapo mashabiki waliokuwepo uwanjani, walikuwa wakisema kuwa, ni
mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kutoka
Morogoro, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro, jana zilianza
ligi kuu Bara kwa kugawana pointi, baada ya kutoka suluhu, katika mechi
iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Katika mchezo huo, washambuliaji wa Mtibwa Sugar,
Jamal Mnyate na Hussein Javu, walishindwa kutumia vizuri nafasi walizopata na
kuinyima timu yao ushindi.
Hivyo, kwa matokeo hayo, timu hizo zote kutoka
mkoani Morogoro, zimeambulia pointi moja.
Kutoka
Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Coastal Union imedhihirisha ubabe wake kwa Mgambo JKT, baada ya
kuilaza bao 1-0, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Bao pekee la Coastal Union lilifungwa na Jerry
Santo, dakika ya 46, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Juma Jabu na
kuukwamisha mpira wavuni.
Kutoka
jijini Mwanza,
Toto Africa na Oljoro JKT, zimegawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1,
katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini
hapa.
Toto walitawala mchezo kipindi cha kwanza, lakini
dakika ya nne walishindwa kufunga bao kwa mkwaju wa penalti, baada ya Emmanuel
Swita kupiga mkwaju huo na kupanguliwa vizuri na kipa Shaibu Issa wa Oljoro
JKT.
Baada ya kukosa penalti hiyo, Oljoro walizinduka na
kulisakama lango la wapinzani wao, ambapo Omar Issa alipata nafasi nzuri ya
kufunga bao, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Toto walipata pigo baada ya beki wake wa kati,
Evarist Maganga kuumizwa mdomoni na kukimbizwa hospitali, nafasi yake
ikachukuliwa na Hussein Shaha.
Oljoro wakijibu mashambulizi, walipata nafasi nzuri
dakika ya 85, lakini shuti la Omar Issa, lilipanguliwa na kipa kipa wa Toto,
Emmanuel Ngwengwe, kabla ya mabeki kuuondoshwa katika hatari.
Mashambulizi ya Oljoro yalizaa matunda dakika ya 87,
baada ya Hamad Omar kuipatia, lakini Mohamed Neto aliisawazishia Toto bao hilo
dakika ya 87.
Kutoka
katika Uwanja wa Azam Chamazi jijini Dar es Salaam,
timu ya soka ya Ruvu JKT, jana ilianza vizuri ligi kuu Bara, baada ya kuilaza
Ruvu Shooting mabao 2-1.
Mechi hiyo ilizikutanisha timu zote zinazomilikiwa
na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambapo kila timu ilionesha kiwango kizuri
uwanjani.
No comments