Simba yaichapa Lyon 3-0
![]() |
Ngassa, kushoto akiwa na Kaseja. |
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba, jana walianza
ligi kuu Bara kwa kishindo baada ya kuigandamiza African Lyon mabao 3-0, katika
mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa mabingwa hao
watetezi, kwani wiki hii tayari ilibeba Ngao ya Jamii, kwa kuifunga Azam FC,
mabao 3-2.
Hivyo, ushindi huo ulikuwa kama kufunguliwa kwa njia
ya ushindi katika ligi hiyo iliyoanza jana kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Simba walifanikiwa kulifikia lango la Lyon, baada ya
Emmanuel Okwi kupokea pasi safi kutoka kwa Daniel Akuffo dakika ya 15, lakini
shuti lake kali lilidakwa kiufundi na kipa Abdul Seif.
Wakichezeshwa vizuri na Mwinyi Kazimoto, washambuliaji
Okwi na Akuffo, dakika ya 29, walionana vizuri, lakini beki Sunday Bakary na
Benedictor Mwamlangala, wanafanya kazi nzuri ya kuondoa hatari langoni kwao.
Dakika ya 34, Okwi aliwainua mashabiki wao wa Simba,
baada ya kufunga bao zuri akitumia vizuri pasi ndefu ya Amri Kiemba iliyompita
beki Johanes Kajuna na kuukwamisha mpira wavuni.
Dakika ya 35, Mwinyi Kazimoto anaunawa mpira ndani
ya eneo la hatari na kuwa penalti iliyotolewa na mwamuzi Oden Mbaga, lakini
Sunday Bakari anapiga mpira na kugonga mwamba wa goli.
Baada ya mpira huo kuogonga mwamba na kurudi
uwanjani, kiungo Kiemba aliuwahi na kupiga pasi ndefu kwa Mrisho Ngassa, ambaye
aliwazidi mbio mabeki wa Lyon na kupiga shuti lililoongezewa kasi na Said
Nassoro ‘Cholo’, dakika ya 36 na kuwa bao la pili.
Dakika ya 58, Hamad Manz alimchezea vibaya Okwi na
kuwa penalti, ambayo ilifungwa na Akuffo na kuwa bao la tatu. Manz alioneshwa
kadi ya njano kwa kosa hilo.
Katika mchezo huo ambao ulikosa msisimko, Simba
walikuwa wakitumia vizuri nafasi walizopata na kufanikiwa kufuynga mabao yote
matatu.
Lyon:
Abdul Seif, Johanes Kajuna/Adam Kingwande, Hamad Manz, Sunday Bakary,
Benedictor Mwamlangala, Sunday Hinju/Hood Mayanja, Obina Salamusasa, Semmy
Kessy, Idd Mbaga/Mohamed Samata, Jacob Masawe, Yusuph Mlipili.
Simba:
Juma Kaseja, Said Nassoro‘Cholo’, Amir Maftaha, Shomari Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi
Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi ‘Boban’/Salum Kinje, Daniel Akuffo/Ramadhan
Chombo, Mrisho Ngassa/Abdallah Juma, Emmanuel Okwi.
No comments