Header Ads

ad

Breaking News

Simba mwendo mdundo


Juma Kaseja (kulia) na Mrisho Ngassa



MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba, wameendeleza wimbi lao la ushindi katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.

Hata hivyo, ushindi huo ulipatikana huku timu hiyo ikiwa pungufu baada ya mshambuliaji wao Mganda Emmanuel Okwi kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 38, baada ya kumpiga kiwiko beki wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.

Pamoja na kumiliki vyema mpira sehemu kubwa ya mchezo huo, JKT Ruvu walishindwa kabisa kuhimili vishindo vya Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Lager, baada ya kujikuta ikilambwa mabao hao mawili.

Kwa ushindi huo wa pili mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani, Simba imefanikiwa kufikisha pointi sita na hivyo kuwa kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Kiungo mkabaji Amri Kiemba, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipatia Simba bao katika dakika ya 47 baada ya shambulizi kali ambapo mabeki wa JKT Ruvu walishindwa kuwa makini kuondosha hatari.

Katika dakika ya 72, Haruna Moshi ‘Boban’, aliipatia Simba bao la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mrisho Ngassa ambaye katika mchezo huo, alionekana kuwa mwiba mkali kwa JKT Ruvu.

Bao hilo lilianzia kwa Ramadhani Chombo ‘Redondo’ ambaye aliingia kuchuku nafasi ya Daniel Akuffo dakika ya 60 ambapo kiungo huyo aliwapangua walinzi wa JKT Ruvu na kutoa pasi kwa Ngassa.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Kagera Sugar ilibanwa na Oljoro JKT kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa suluhu, huku Toto African ikipata sare ya mabao 2-2 na Azam Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Ruvu Shooting iliichapa Mgambo JKT mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mjini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine, Prisons ya huko ilitoka sare ya bao 1-1  na Coastal Union ya Tanga, wakati kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, African Lyon iliichapa Polisi Moro bao 1-0.

No comments