Masikini Yanga, yalambishwa sukari mara tatu
![]() |
Yanga |
*Mtibwa kiboko yao, Mecky alonga
MBWEMBWE za usajili na kelele za mitaani, si lolote
uwanjani. Kauli hiyo ilitimia jana baada ya
Yanga, kukubali kipigo cha mabao 3-0, dhidi ya Mtibwa Sugar, katika
mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Timu zote mbili zilianza mchezo huo kwa
kushambuliana, lakini Mtibwa Sugar ndio waliokuwa wa kwanza kulifikia lango la
Yanga na kumsalimi kipa Ali Mustapha Barthez.
Juhudi za Mtibwa Sugar ambao walikuwa wakiutumia
uwanja wa nyumbani wa Jamhuri, zilizaa matunda dakika ya 12, baada ya Dickson
Daud kuifungia timu yake bao kwa kichwa, akitumia vizuri mpira wa kona
uliopigwa na Malika Ndeule.
Mtibwa wakiwa na nguvu baada ya kupata bao,
walifanikiwa kulitia msukosuko lango la Yanga, baada ya Hussein Javu kupiga
shuti kali lililogonga nguzo ya goli.
Pamoja na juhudi za Yanga kutafuta bao la
kusawazisha, walijikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 43, lililofungwa na
Javu, akitumia vizuri makosa yaliyofanywa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na
kuusindikiza mpira kimiani.
Yanga, ambao katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa
ligi waliyocheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mkoani Mbeya, ilitoka
suluhu na Prisons ya Mbeya, ilibanwa vizuri na wakata miwa wa Mtibwa kipindi
chote cha kwanza.
Kipindi cha pili kmilianza kwa Yanga kuliandama
lango la Mtibwa, ambapo dakika ya 51, Athuman Idd ‘Chuji’, alikosa bao, baada
ya shuti lake kuokolewa kwa miguu na kipa Shaaban Kado.
Didier Kavumba aliyeingia kuchukua nafasi ya Mbuyu
Twite, alipata nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 74, lakini alishindwa
kuunganisha vizuri mpira wa krosi uliopigwa na Hamis Kiiza na kutoka nje.
Wakiwa bado wameduwaa kwa kukosa bao, Yanga,
walijikuta wakichapwa bao la tatu dakika ya 76, lililofungwa na Javu, ambaye
alikuwa akiisumbua ngome ya vijana wa Jangwani.
Dakika ya 84, Haruna Niyonzima, alipata nafasi nzuri
ya kufunga, lakini mpira aliopiga ukielekea wavuni, uliokolewa na beki Daud.
Yanga walipata penalti dakika za mwisho za mchezo iliyotolewa
na mwamuzi Mathew Akram kutoka jijini Mwanza., lakini mkwaju uliopigwa na Kiiza
ulipaa juu ya lango la Mtibwa Sugar, baada ya beki Malika Ndeule, kuunawa mpira
ndani ya eneo la hatari.
Wakati Yanga wakiugulia kipigo, Kocha Mkuu wa Mtibwa
Sugar, Mecky Mexime, alisema kuwa, ahadi aliyoitoa ya kuifunga Yanga, imetimia,
ingawa wapinzani wana kocha wa kigeni mwenye uzoefu wa kufundisha soka.
“Vijana wangu walicheza vizuri na walistahili
ushindi, kelele za mwamuzi alikuwa upande wao, lakini hilo hatulilalamikii,
kazi yetu imetimia,” alisema.
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet, alisema
kuwa, waamuzi wa mchezo huo walichezesha vizuri, lakini vijana wake ndo wa
kulaumiwa kwa kushindwa kuzitumia vizuri nafasi walizopata.
Kocha huyo aliimwagia sifa Mtibwa Sugar, kuwa ni
timu nzuri na ilicheza vizuri vipindi vyote viwili, lakini kwa upande wao,
alisema wanatakiwa wajiulize wenyewe.
Mtibwa:
Shaaban Hassan ‘Kado’, Malika Ndeule, Issa Rashid, Dickson Daud, Salvatory
Ntebe, Shaaban Nditi, Januari Mnyange, Awadh Juma, Hussein Javu, Shaaban
Kisiga, Vicent Barnabas.
Yanga:
Ali Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Mbuyu Twite/Didier Kavumbagu, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo/Simon Msuva,
Haruna Niyonzima, Said Bahanunzi, Hamis Kiiza, David Luhende.
No comments