Familia ya Mafisango yatupiwa virago nje
Mdogo wake, Joel Mafisango akiangalia vyombo vyao. |
Na Mwandishi Wetu
FAMILIA ya
aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu ya Mabingwa wa soka Ligi Kuu Bara,
Patrick Mutesa Mafisango, jana wamejikuta wakitupiwa vitu vya marehemu
Mafisango nje ya nyumba hiyo kwa kudai kuwa mkataba wa kuishi hapo umekwisha.
Familia hiyo imejikuta ikiwa katika wakati mgumu
baada ya mkataba wa kuishi katika nyumba ambayo marehemu Mafisango alikuwa
anaishi kumalizika ambapo ilidaiwa kulipwa na uongozi wa Simba.
Akizungumza na SuperStar jana, ndugu wa marehemu
Mafisango, Joel Mafisango, alisema kuwa, kitendo kinachofanywa na uongozi wa
Simba, si kizuri cha kuzuia kuuza mali za marehemu wakiwa kama ndugu wa
marehemu.
“Uongozi wa Simba kutuzuia ndugu wa marehemu kuuza
vitu si vizuri, sisi ni watu ambao tulikuwa tunaishi na marehemu na ni ndugu,
iweje watuzuie kufanya hivyo,” alisema.
Alisema kuwa, kama Simba hawapo tayari kuruhusu
kuuza vitu hivyo, basi wavisafirishe mpaka nyumbani kwa marehemu ili na wao
waweze kuondoka, kwani wanaishi kwa shida.
“Kama wanatuzuia kuviuza vitu, tunaomba wawe na
jukumu la kuvisafirisha mpaka nyumbani kwao marehemu, tunakaa hapa sababu ya
vitu vya marehemu, ingawa Simba hawatujali, wala kufikiria mali za marehemu,
mchezaji wao.
“Tunadhalilika kwa sababu ya timu ya Simba, na kama
hawatafanya hivi ambavyo ndugu tunahitaji, basi wajue lazima watakwenda kwenye
kaburi la marehemu Mafisango kule DR Congo kuomba msamaha, juu ya kaburi, kwa
kitendo ambacho wametufanyia, vingenevyo Simba haiwezi kufika kokote
kimaendeleo,” alisema Joel ambaye alionekana kusononeshwa na kitendo hicho.
Naye mmiliki wa nyumba hiyo, Chingweni Mtoro,
alisema kuwa, mkataba wa marehemu Mafisango ulikuwa umemalizika Julai 28, mwaka
huu na kudai kuwa, uongozi wa Simba
uliomba kuongezewa muda wa siku saba, ili waweze kushughulikia suala hilo.
“Julai 28, mwaka huu ndio ilikuwa mwisho wa mkataba,
lakini baadhi ya wahusika wa Simba SC, akiwemo Kesi aliyemtaja kwa jina moja,
alimwomba waongeze muda wa siku saba ili waweze kulipa kodi ya mwezi mmoja
mbele.”
“Mpaka kufikia sasa, kila nikijaribu kuongea na
uongozi huo kwa njia ya simu, naambiwa subiri, na huu ni mwezi wa nane, sioni mwelekeo wowote wa kupewa change, hivyo
naona bora niwafukuze ndugu wa marehemu Mafisango,” alisema.
Alisema kuwa, kwa sasa amepata mtu mwingine anayetakiwa
kuingia kwenye nyumba hiyo, na ndio maana ameona njia pekee ni kuwaondoa ndugu
hao.
“Kama wapo tayari kuondoka, nipo tayari kuwasaidia
usafiri wa kubebea mizigo yao na kuipeleka kule ambako watakwenda kuishi kwa
hapa Dar es Salaam, na hilo deni langu la sh. 350,000, ambalo ni la mwezi mmoja,
nitawasamehe,” alisema Mtoro.
Familia hiyo ilikuwa ikiishi na marehemu Mafisango
ambaye alifariki April mwaka huu, alikuwa akiishi na ndugu zake wanne akiwemo
Joel.
Katika kujua ukweli wa jambo hilo, gazeti hili liliweza kuzungumza na uongozi wa
Simba kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wao,
Geofrey Nyange ‘Kaburu’, ambaye alikiri kwamba,
mkataba wa pango kwenye nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Keko jijini Dar es
Salaam, umekwisha na kuwataka ndugu hao kurejea kwao kama hawana kazi ya
kuwawezesha kuishi.
“Tunaweza kuwasaidia, lakini si wajibu wetu, notisi
ilitoka na kati ya hao mmoja ambaye ni ndugu wa Mafisango, alikwenda hadi
Kinshasa kuzika, lakini wengine ni ndugu wa kuunga unga na wanatoka maeneo ya
Goma.
“Jambo la msingi warudi makwao kama hapa hawana kazi ya kuwawezesha
kuishi mjini, huyo wa Kinshasa ambaye ni ndugu wa marehemu tutampa nauli kama
akiwa tayari kwa muda wake. Tatizo hawataki kurudi kwao na wanataka Simba iwape
nyumba na fedha ya chakula, je, yanawezekana hayo? Alihoji Kaburu.
No comments