Nizar Khalfan atua rasmi Simba
![]() |
Nizar Khalfan |
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Nizar Khalfan aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa Marekani, amejiunga rasmi na vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu, Simba.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, usajili wa mchezaji huyo umefanikishwa na mmoja wa wafadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji.
Dewji mwenyewe alipotafutwa kuzungumzia hilo, alikiri na kusema kuwa, aliombwa na uongozi wa Simba kufanikisha usajili wa mchezaji huyo na kwamba, baada ya kufanikiwa, amemkabidhi mchezaji huyo kwa uongozi wa klabu.
"Kama mwana-Simba, nimetimiza wajibu wangu kama nilivyoombwa na uongozi. Nimeambiwa ataungana na wenzake kuanza mazoezi wakati wowote kuanzia Jumatatu (leo)," alisema na kuongeza kuwa, mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Moro United atakuwa na nafasi ya kuanza kuichezea Simba katika michuano ya kimataifa mwaka huu endapo itaingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Baada ya kuzing'oa ya Kiyovu ya Rwanda na Setif ya Algeria, wiki hii Simba itaishukia Al Ahly Shandy ya Sudan na kama ikifanikiwa kuvuka kiunzi hicho, itaingia katika raundi nyingine itakayoamua timu za kucheza hatua ya Nane Bora Afrika.
Habari zaidi zinasema kuwa, Nizar leo atakabidhiwa rasmi jezi atakayoitumia akiwa Simba, muda mfupi kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Moro United unaotarajiwa kuanza saa kumi alasiri.
Mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutajwa jina akisema si msemaji, alikiri kukamilika kwa taratibu za Nizar kutua Simba, huku akiongeza kuwa, ataisaidia klabu hiyo katika michuano ya ligi na ile ya kimataifa kuanzia msimu ujao.
"Ni kweli, timu inazidi kuimarika. Kumpata staa wa kimataifa kama Nizar ni jambo la kujivunia, tunashukuru kwa juhudi zilizofanyika na hatimaye kumpata mchezaji huyu," alisema.
Nizar ambaye Juni 21, mwaka huu atatimiza umri wa miaka 24, kabla ya kutua Simba aliichezea Philadelphia Union ya Ligi Kuu ya Marekani aliyodumu nayo kwa miezi mitatu tu baada ya kujiunga nayo akitokea Vancouver Whitecaps. Alikuwa Vancouver tangu Agosti 22, mwaka 2009 akitokea Moro United.
Katika soka ya ushindani, nyota huyo aliibukia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2004 na baadaye akajiunga na Mtibwa Sugar kabla ya kutimkia Kuwait kuichezea Al Tadamon ya huko msimu wa 2007-2008. Kutoka Tadamon alikwenda Lebanon na kuichezea Tadamon Sour ya huko na mwaka 2009, aliichezea Moro United.
No comments