Header Ads

ad

Breaking News

Wabunifu kuonesha mambo Swahili Fashion Arusha Jumamosi


WABUNIFU 15 wa mavazi nchini, watafanya onesho la mavazi katika uzinduzi wa 'Swahili Fashion Week' Oktoba 8 mwaka huu katika hoteli ya Mount Meru ya Jijini Arusha.

Uzinduzi huo pia utafanyika Jijini Dar es Salaam Novemba 10 hadi 12, mwaka huu katika Ukumbi wa makumbusho ya Taifa.

Mwandaaji na Mwanzilishi wa Swahili Fashion Week, Mustapha Hasanali amesema wamedhamiria kupeleka maonesho hayo kwa mara ya kwanza Arusha kwa kuwa ni makao makuu ya nchi za Afrika Mashariki, kwa kuwa itasaidia kueneza zaidi maonesho hayo kwa nchi zinazozungumza lugha ya kiswahili.

Amesema hatua hiyo imefikiwa mwaka huu, baada ya kufanya maonesho hayo kwa miaka mitatu mfululizo Dar es Salaam na kwamba hiyo itapanua wigo wa maonesho ya mavazi ya Swahili na kukuza mavazi ya Tanzania na watu wanaoishi katika nchi zinazozungumza kiswahili.

Hasanali amesema kwa mara ya kwanza Swahili Fashion Week, wameandaa tuzo 16 zitakazoshindaniwa kupitia vipengele mbalimbali na hiyo inalenga kutoa changamoto kwa wadau wote wanaoshiriki katika masuala ya ubunifu na mitindo.

Amezitaja baadhi ya tuzo zitakazoshindaniwa ni mbunifu bora wa mwaka, mbunifu bora wa mavazi anayechipukia, mwanamitindo bora wa mwaka wa mitindo wa kike, mwanamitindo bora wa mwaka wa kiume pamoja na tuzo nyingine.

Amesema mbali na tuzo hizo pia maonesho hayo yatashirikisha wabunifu chipukizi, ambao watashindania tuzo ya mbunifu bora na mwanamitindo bora chipukizi.

Mwandaaji huyo amesema maonesho hayo yamedhaminiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Southern Sun, Precision Air, Amarula, Ultimate Sucurity, Redd's, Image Master Global Outdoor, Vayle Springs, Eventlites na 361 Degrees.


 

No comments