So Kalnery, Jhiko Man kuwanoa wanamuziki Zanzibar
Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, Imma Mbuguni (kushoto) akiangalia CD ya msanii, So Kalmery wakati alipotembelea ofisi za gazeti hili, Dar es Salaam jana. Kulia ni Msanii, Jhikolabwino Manyika (Jhikoman).Foto: Rajabu Mhamila.
MWIMBAJI nguli wa muziki wa reggae nchini, Jhikolambwino Manyika 'Jhiko Man na So Kalmery kutoka Ufaransa, wataendesha mafunzo ya muziki kisiwani Zanzibar hivu karibuni.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili mjini Dar es Salaam, Jhiko Man alisema kuwa, watafanya onesho kisiwani Zanzibar na mafunzo ya kwa wanamuziki wa kisiwani humo.
Mwimbaji huyo wa muziki wa raggae, alisema kuwa, amemwalika Kalmery nchini ili kutoa mafunzo kwa wanamuziki mbalimbali.
"Huyu mzee ni mwanamuziki aliyebobea sana, anaufahamu muziki wa aina mbalimbali, hivyo itakuwa nafasi nzuri kwa wanamuziki," alisema.
Jhiko Man alisema mwanamuziki huyo anayeimba kwa lugha ya kiswahili, anafanya kazi yake ya muziki nchini Ufaransa.
"Kikubwa mgeni wetu atawaonesha safari ya muziki inavyokuwa, njia zake mpaka kufikia mafanikio, hilo litakuwa somo zuri kwa wanamuziki wetu," alisema.
Mpiga raggae huyo, alisema kuwa, kwasasa anapiga muziki wa brakka unaofanana kidogo na hip hop, lakini ukiwa na vionjo halisi vya kitanzania.
Naye, Kalamery, alisema kuwa, nafasi aliyopata ya kufika nchini, ataitumia vizuri kuwafundisha wanamuziki wengine ambao hawajapata mafunzo ya muziki.
"Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuwapa kile nilicho nacho ili nao waweze kufika juu zaidi kimuziki," alisema.
Mwanamuziki huyo aliyezaliwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), eneo la Bukavu, alianza safari ya muziki miaka mingi na kufanikiwa kufanya kazi na Mbaraka Mwinshehe.
Kwa sasa mwamuziki huyo anaishi nchini Ufaransa, ambapo hufanya kazi zake nchini humo na kuzungunguka mataifa mbalimbali ya Ulaya na Amerika.
No comments