Salum Kabunda ninja afariki, azikwa Mwanza
Katika picha: Toka kushoto ni Hamis Gaga ‘Gagarino’(marehemu), Saidi Mwamba ‘Kizota(marehemu), David Mwakalebela, Method Mogella(marehemu), Abeid Mziba, Ken Mkapa, Na Salum Kabunda ‘Ninja’. Nyuma kwa mbali ni Stephen Nemes. Ilikuwa mwaka 1992.
MCHEZAJI wa zamani wa Yanga, Salum Kabunda amefariki dunia nyumbani kwa kaka yake jijini Mwanza, usiku wa kuamkia jana.
Kabunda aliyewahi kuvuma na mabingwa soka nchini, akitokea Tukuyu Stars ya Mbeya, amefariki baada ya kuugua kwa muda wa mwezi mmoja alipoanza kutibiwa katika Hospitali ya Msikiti wa Ijumaa iliyopo ya Mwanza.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina kwa kusema si msemaji wa familia, kilisema kuwa, kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibu, marehemu alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu ya kushuka na kisukari.
Kabunda alizikwa jana mchana katika makaburi ya Kitangiri mjini Mwanza.
Baada ya kustaafu soka, Kabunda alikuwa ni wakala wa magari katika masuala ya Bima na kutoa magari bandarini jijini Dar es Salaam.
Kifo cha Kabunda kimeacha pengo kubwa jijini Mwanza, mpaka sasa limepoteza wanasoka wakongwe watatu, Anthony Nyembo, Beya Simba na sasa Salum Kabunda.
Katika uhai wake, mwaka 1986, alikuwa Tukuyu Stars, lakini aliihama timu hiyo na kujiunga na Yanga mwaka 1988. Pia, alizichezea timu za Taifa ya kakakuona mwaka 1992 na baadaye timu ya Taifa Taifa Stars.
No comments