Header Ads

ad

Breaking News

Maproo Stars kukamilika Jumanne

 
Mshambuliaji wa timu ya Taifa Mrisho Ngasa (kushoto), akimtoka nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa, wakati wa mazoezi kwa timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam leo. Foto:  Zuberi Mussa.


KIUNGO wa timu ya Vancouver WhiteCaps ya Canada na timu ya Taifa 'Taifa Stars', Niza Khalfan atatua nchini Jumatatu kuungana na wenzake kujiandaa na mechi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Africa mwakani dhidi ya Morocco mjini Marakech.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, leo amesema walituma barua Vancouver, hawajapata taarifa nyingine, hivyo wanatarajia Nizar atawasili kesho.

"Tulituma barua kwenye klabu anayocheza Nizar, hatujaelezwa lolote, hivyo inaonesha hakuna tatizo, Nizar atawasili Jumatatu," amesema Wambura.

Wambura amesema mbali na Nizar, wengine watakaowasili Jumatatu ni Henry Joseph anayechezea klabu ya Kongsvinger ya Norway na Athuman Machupa anayekipiga katika klabu ya Vasalund ya Sweden.

Amewataja Danny Mrwanda na Abdi Kassim 'Babi', wanaochezea timu ya DT Long ya Vietnam kuwa, watawasili Jumanne na kujiunga na wenzao kambini.

Wambura amesema wachezaji wawili wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, Idrissa Rajab wa Sofapaka ya Kenya na Mbwana samatta anayekipiga TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), watawasili kesho nchini.

"Jumanne, kikosi cha Stars kitakuwa kimekamilika, na Kocha Jan Poulsen, atakuwa na wakati mzuri wa kukamilisha programu yake kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco," alisema.

Wachezaji wengine walioitwa Stars na kuanza kambi ni Juma Kaseja, Shaban Kado na Shaban Dihile (makipa), Shadrack Nsajigwa, Aggrey Morris, Juma Jabu, Juma Nyosso, Erasto Nyoni na Victor Costa kwa upande wa mabeki.

Viungo ni Joseph, Shaban Nditi, Nurdin Bakari, Kassim, Ramadhan Chombo, Nizar, Jabir Aziz, wakati wafumania nyavu ni Hussein Javu, Mrisho Ngassa, John Bocco, Samatta, Machupa na Mrwanda.

Stars na Morocco zitaumana Oktoba 9, mwaka huu mjini Marakech.

No comments