Header Ads

ad

Breaking News

Nchimbi awaeleza ukweli viongozi wa michezo



WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Emmanuel Nchimbi, amesema hali ya michezo iliyopo sasa nchini ni mbaya na sababu iliyosababisha ni viongozi kulipaka rangi jambo hilo.

Waziri Nchimbi, amesema hayo Dar es Salaam leo wakati akizindua Baraza jipya la Michezo la Taifa (BMT), aliloliteua wiki iliyopita.

Katika uzinduzi huo, Nchimbi amewataka viongozi aliowateua kuanza majukumu yao, huku wakitambua kuwa, hakuna mchezo hata mmoja unaoridhisha hadi sasa.

Amewashauri viongozi hao wa BMT chini ya Mwenyekiti mpya Deoniz Malinzi, kuandaa mpango na mfumo mpya wa utendaji wa kazi ambao utasaidia hata kuishawishi Serikali, kuiongezea bajeti wizara hiyo ambayo kwa sasa pato lake ni dogo, ikilinganishwa na baadhi ya wizara zingine.

Waziri huyo amewataka wajumbe na viongozi wa baraza hilo, kushirikiana kikamilifu na vyama vya michezo katika kazi zao za kila siku, ili kujenga mahusiano yenye tija na kuimarisha hali ya michezo nchini.

Nchimbi amesema kufanya kazi kwa kutambua mfumo wa taasisi za kuibua vipaji na kuzingatia ushirikiano na majeshi ya ulinzi na usalama kutokana na jitihada zao nzuri, huku akitolea mfano Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Malinzi kwa upande wake, alimshukuru Waziri Nchimbi kwa kuteua baraza hilo na kumhakikishia kuwa limeanza kufanya kazi yake rasmi, mara baada ya uzinduzi huo mapema jana.

Amesema amesikitishwa kuona Tanzania, ambayo ina zaidi ya watu milioni 40 haina mchezo hata mmoja, ambao unafanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, jambo ambalo watalifanyia kazi.

No comments