Mtibwa Sugar yaididimiza Villa Squad
TIMU ya Mtibwa Sugar, jana iliichapa Villa Squad mabao 2-0, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
Mtibwa walianza mchezo kwa kulisakama lango la wapinzani wao na kujipatia bao la kwanza lililofungwa na Thomas Mourice kwa shuti kali lililojaa wavuni.
Villa Squad walishindwa kufurukuta mbele ya Mtibwa na kuwaacha watawale dakika zote za mchezo.
Dakika ya 49, Said Rashid aliiongezea bao la pili Mtibwa Sugar baada ya kuunganisha vizuri mpira wa krosi uliopigwa na Masoud Ally na kumpiga chenga kipa Mohamed Bambino.
Kutoka Mlandizi, timu ya Ruvu Shooting iliibuka na mabao 2-1, dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mlandizi.
Bao la kwanza la Ruvu Shooting lilifungwa na Ayoub Kitala dakika ya 14, bao la pili lilifungwa na Seif Abdallah dakika ya 19.
Coastal ilijipatia bao lake kupitia kwa Salim Gila dakika ya 38, baada ya kumzidi ujanja kipa Benjamini Haule.
Kutoka Mwanza, mechi kati ya Toto African na JKT Ruvu zilizoumana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, zimetoka suluhu.
No comments