Watanzania watakiwa kuchangamkia uwekezaji
Aderina Rushekya, Kaimu Meneja Mawasiliano Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania
Na Mwandishi Wetu, Kwala
WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia uwekezaji, badala ya kukaa pembeni huku fursa hiyo wakiiacha kwa raia kutoka nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa na Aderina Rushekya, Kaimu Meneja Mawasiliano Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania, alipozungumza na waandishi wa habari eneo la Kwala unakotekelezwa mradi wa kongani la viwanda.
Alisema kuwa serikali imetoa kipaumbele kwa watanzania katika sekta hiyo, ambapo mzawa anapaswa kuwa Dola milioni 5 sawa na Sh.bilioni 12.5, huku raia wa kigeni akitakiwa kuwa na Dola milioni 10 sawa na Sh.bilioni 25.
Aliongeza kuwa sababu za kuwapatia kipaumbele wazawa ni fursa ya rasilimali zote zitabaki nyumbani, tofauti na raia kutoka nje ya nchi, ambaye fedha atazipeleka kwao.
"Kwa wawekezaji wazawa pamoja na kwamba, wote watapatiwa ardhi pasipokuwa na malipo, wazawa rasilimali zote zitabaki nyumbani tofauti na wageni," alisema Rushekya.
Akizungumzia uwekezaji zaidi, Rushekya alitaja maeneo mengine ambayo yameandaliwa ni Bagamoyo, NALA iliyopo Dodoma na Buzwagi Shinyanga.
Naye, Gerald Thilia, Meneja Msaidizi wa Kampuni ya SNOWSEA, inayojihusisha na utengenezaji wa majokofu (friji), za aina na ukubwa tofauti alisema kuwa, walipatiwa ujuzi na Wachina, ambao wameondoka na kwamba, amebaki mmoja kwa ajili ya shughuli za kitaalamu zaidi.
No comments