'Jela' miezi sita kwa kubomoa ukuta
‘Jela’ miezi 6 kwa kubomoa ukuta mkazi wa Kigamboni, Moran Milan, amehukumiwa kifungo cha nje miezi sita baada ya kupatikana na hatia ya kubomoa uzio wa ukuta jirani na anapolinda na kusababisha hasara ya Sh. milioni 5.5.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mwanzo Kigamboni, Christina Luguru, amesema mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashitaka umethibitisha shitaka dhidi ya Milan bila kuacha shaka.
Ilidaiwa kuwa usiku wa Julai 10, 2024 eneo la Kimbiji, Wilaya ya Kigamboni, mshitakiwa na wenzake ambao walitoroka walivamia na kubomoa uzio uliozungushiwa kwenye nyumba inayomilikiwa na kampuni ya Baywarch bila ruhusa ya mmiliki. “Kosa alilofanya mshitakiwa ni baya na kamwe halivumiliki kwenye jamii.
Ili mshitakiwa na wengine wenye tabia kama hii wapate fundisho, atatumikia kifungo cha nje chini ya huduma kwa jamii kwa muda wa miezi sita,” alisema hakimu. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Baywarch, Lilian Kileo, aliiambia mahakama kuwa alijulishwa usiku wa tukio kuwa vijana wa ‘kiamasai’ akiwamo mshitakiwa ambaye alimfahamu kabla ndio waliofanya uharibifu huo.
Shahidi mwingine, Sylivester Gohagi aliiambia mahakama kuwa alimtambua mshitakiwa aliyekuwa amevaa mavazi ya kimasai akishirikia kubomoa uzio huo na kwamba alimfahamu mshitakiwa kabla ya tukio hilo.
Mshitakiwa ambaye alikana shitaka hilo aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio aliondoka kazini kwake ambapo ni Jirani ya ukuta ulioharibiwa saa 12 jioni na aliporudi jioni alikuta ukuta huo unaopakana na eneo analolinda umevunjwa.
“Kwa ushahidi uliotolewa mahakama inajiridhisha kuwa upande wa mashitaka umeweza kuthibitsha shitaka bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa ndiye aliyetenda kosa hilo na anatiwa hatiani,” alisema Hakimu Lugulu.
Baada ya kutiwa hatiani mshitakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na ana familia inayomtegemea.
No comments