Header Ads

ad

Breaking News

Watu 484 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo maonesho ya madini Geita

Wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wakifurahia baada ya kupokea tuzo ya mshindi wa pili kwa taasisi zinazotoa huduma ya afya wakati wa kufunga maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Geita.


Na Mwandishi Maalumu - Geita

WATU 484 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya nane ya kitaifa ya madini yaliyokuwa yanafanyika katika viwanja vya maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Henry Mayala, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma walizokuwa wanazitoa kwenye maonesho hayo.

Dkt. Mayala alisema kati ya watu 484 waliofanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo 473 walikuwa watu wazima na 11 walikuwa watoto ambapo wengi wao wamekutwa na shinikizo la juu la damu, kisukari na uzito uliopitiliza.

“Wengi walikuwa hawajui kama wana haya matatizo kwahiyo kitendo cha kupima afya kimeweza kuwasaidia kupata matibabu mapema na elimu itakayowasaidia kujikinga na magonjwa hayo,” alisema Dkt. Mayala.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Henry Mayala, akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mkazi wa Geita aliyefika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zikitolewa katika maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini na kumalizika hivi karibuni mkoani Geita.

Dkt. Mayala alitoa wito kwa wananchi waweze kujitokeza kwa wingi pale wanaposikia taasisi hiyo ikitoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo ili kutibiwa mapema.

Nao wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika maonesho hayo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa zimwewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata matibabu.

“Huduma ipo vizuri ukifika unapimwa kwa dakika chache tu na huchelewi na vipimo vyao ni bure na madaktari wanatupa ushauri mzuri wa kujua afya zetu,” alisema Dayness Lucas mkazi wa Fadhili Bucha Geita.

“Nimepimwa presha na kisukari bure na nimepewa ushauri huu ni msaada mkubwa kwa kuwa vipimo hivi ni vya gharama kubwa lakini hapa tumepata bure,” alisema Neema Robin mkazi wa Geita.

“Kwa mfano, huu upimaji wa moyo kikawaida ilikuwa kupata huduma yao ni mpaka uende Dar es Salaam, lakini sahivi tunapata hapa karibu,” alisema Neema Robin mkazi wa Geita.

Katika maonesho hayo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilishika nafasi ya mshindi wa pili katika kundi la taasisi inayotoa huduma ya afya.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aisha Ally Said, akimsikiliza mkazi wa Geita aliyefika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt.Samia Suluhu Hassan kupatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Geita.

Wananchi wa mkoa wa Geita wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Geita. Picha na: JKCI


No comments