Msajili wa Vyama azungumzia Maalim Seif Sharif Hamad kufungua ofisi mpya za CUF

Kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) kufungua ofisi mpya za chama
hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni, Magomeni wilaya ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa amesema
anaamini chama hicho kinafanya mambo yake kwa kuzingatia sheria.
Jana Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema
hajapata taarifa yoyote ya chama hicho, kufungua ofisi mpya zaidi ya
kuona katika vyombo vya habari.
“Ukiondoa taarifa za kwenye media sijapata taarifa yoyote kutoka
CUF labda wawe wameleta leo (jana), lakini naamini chochote
wanachofanya wanaelewa taratibu wataleta taarifa, “ alisema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi alisema sheria inawataka wanapofungua ofisi watoe
taarifa ndani ya siku 14, ambazo hazijaisha hivyo anaamini wanajua hilo.
Upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad wamefungua ofisi
hizo, baada ya tukio la kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Buguruni na kundi
la Profesa Ibrahim Lipumba.
Jaji Mutungi alisema atakapopokea taarifa rasmi ataangalia kama
taratibu zilifuatwa kwani ufunguaji wa ofisi mpya una taratibu zake.
“Nikiletewa taarifa ndio nitajua kama walifata taratibu au la, ufunguaji wa ofisi una taratibu zake najua wanazijua pia, “ alisema Jaji Mutungi.
Alisema taarifa hiyo ataipata kutoka kwa mwenyekiti au msemaji wa
chama, ambaye ni katibu mkuu ambao wanatambuliwa na ofisi ya msajili wa
vyama vya siasa.
Akizindua ofisi hiyo Juni 4 mwaka huu, Maalim Seif alisema ofisi hiyo imetolewa na wabunge 40 wa CUF.
Alisema uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni kitendo cha kiungwana na kiungwe mkono na wanachama wote.
Alisema kwa miezi 10 sasa, wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa
upande wa Tanzania Bara, jambo ambalo limewaathiri hivyo kupatiwa ofisi
kutamsaidia kutimiza majukumu bila hofu yoyote.
Katibu huyo alisema ana imani na mahakama kuwa itawapatia haki stahiki hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuwa na subira.
No comments