SIMBA, WAGANDA SASA KUCHEZA JUMAPILI
![]() |
Simba |
Mechi
ya Simba na URA ya Uganda kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati
(Kombe la Kagame) iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa
itafanyika Jumapili (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefanya
mabadiliko hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa
ichezwe kwenye uwanja huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Kutokana
na mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10
kamili jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti
itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa Chamazi.
Pia
siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi
nyingine itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu
za Azam ya Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mechi
za ufunguzi wa mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi
ya kwanza saa 8 mchana itakuwa kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya
Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni Yanga itaoneshana kazi na
Atletico ya Burundi.
No comments