Simba gonjwa lile lile
![]() |
Simba wakiwasalimia wachezaji wa URA, kabla ya kuanza kwa mechi, leo. |
*Yatandikwa mabao 2-0 na URA
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba, jana walianza
vibaya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), baada ya
kukubali kipigo cha mabao 2-0, dhidi ya Kodi ya Mapato Uganda (URA), katika
mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, ambao ulianza kwa kila timu
kulisakama lango la wenzake, dakika ya nane, Mwinyi Kazimoto wa Simba alipata
nafasi nzuri, lakini shuti lake kali lilitoka nje ya lango la wapinzani wao.
Ali Feni wa URA, aliipatia timu yake bao la kwanza
dakika ya 11, kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira uliitoka kwa Owen Kasule,
akimwacha kipa wa Simba Juma Kasema akiruka bila mafanikio.
Wakicheza kwa kujiamini, URA ilipata nafasi nyingine
nzuri dakika ya 13, wakati Robert Ssentogo alipomjaribu Kaseja kwa shuti kali
lililopita karibu na lango la Simba.
Danny Mrwanda alishindwa kutumia vizuri pasi iliyotoka
kwa Mussa Mudde, baada ya kubaki na kipa wa URA, Yassin Mugabi na kupiga shuti
lililotoka nje ya lango.
Simba walizidisha mashambulizi, ambapo dakika ya 38,
Mudde alimjaribu kwa shuti la mbali kipa wa URA, Mugabi, ambaye alilipangua,
lakini Mrwanda alichelewa kuufuata mpira na kumpa nafasi kipa huyo kuudaka.
Dakika ya 55, Felix Sunzu wa Simba, alipata nafasi
nzuri, lakini alishindwa kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Abdallah Juma
aliyeingia kuchukua nafasi ya Mrwanda.
Simba wakijitahidi kuongeza mashambulizi ya kusaka bao
la kusawazisha, walijikuta wakichapwa bao la pili dakika ya 88, lililofungwa na
Ali Feni kwa kichwa akiunganisha mpira uliopigwa na Simeon Masaba aliyemtoka
Amir Maftah na kumpasia mfungaji wa bao hilo.
Kipigo hicho ni sawa na kile walichokipata watani wao
wa jadi Yanga, baada ya kuchapwa na Atletico ya Burundi mabao 2-0. Hivyo,
vigogo hao hakuna wa kumcheka mwenzake.
Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amir Maftah, Obadia
Mungusa, Juma Nyoso,Mussa Mudde, Felix Sunzu, Amri Kiemba/Uhuru Seleman, Mwinyi
Kazimoto, Danny Mrwanda/Abdalla Juma, Kanu Mbiyavanga/Haruna Moshi ‘Boban.
URA: Yassin Mugabi, Simeon Massa, Alan Munaaba,
Derrick Walulya, Samuel Ssenkoomi, Oscar Agaba, Ali Feni, Owen Kasule/Augustine
Nsumba, Ssentongo, Said Kyeyune/ Sula Bagala, Yayo Lutimba/Farouk Wejuli.
Kutoka Uwanja wa Azam Chamazi, wamiliki wa uwanja huo,
Azam FC, jana ilishindwa kuutumia vizuri uwanja wake, baada ya kulazimishwa
sare ya bao 1-1 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar.
Katika kundi, URA inaongozwa ikifuatiwa na Azam na
Mafunzo, huku Simba ikiwa ya mwisho.
cio
No comments