Sunday, September 14, 2025

Wakazi Winde wayashangazwa na mawe yaliyopandwa

Na Omary Mngindo, Bagamoyo

WAZAWA wa eneo la Winde Kitongoji cha Mkwajuni Kata ya Makurunge Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameshangazwa kuona mawe yaliyopandwa katika Ardhi yao kiholela.

 Wakizungumza katika mkutano waliouitisha kujadili mambo mbalimbali ya kimaendeleo, walisema hilo ni eneo lao na tayari baadhi yao wamefuata taratibu za kupima kisheria huku wakishangazwa kuyaona mawe ndani ya eneo hilo. 

Akizungumza katika mkutano huo, Muharami Seleman, alisema kuwa eneo hilo ni mji wa kale wenye historia kubwa, huku akieleza kwamba kuna haja ya kuuenzi kwa kuurasimisha kisha kuwekwa huduma za kijamii. 

"Moja ya vitu vya kihistoria ni uwepo wa kaburi la tangu mwaka 1,532 la mtu mweusi, vikiwemo visima vya maji ambavyo vinaendelea kutumika hadi hivi sasa," alisema Seleman.

 Aliongeza kuwa, "Eneo hilo pia ni maarufu kama namba 56, kuna mji ambao umezama baharini, hii inatokana na kupakana na bahari ya Hindi, magofu ya kale, vyungu vya kupikia na maeneo kwa ajili ya masuala ya mila na tamaduni," alisema. 

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa mji huo ulitambuliwa na Waingereza na kwamba, katika ramani ya maeneo yaliyotawaliwa unaonekana, waliourithi kwa wazee wao wenye kaya 45, watu 4,500 kutoka vizazi vilivyotokana na wazee wa eneo hilo ukiwa na hekta 6,000. 

Miraji Miraji ni miomgoni mwa viongozi wa wana Winde alisema kuwa, amefuatilia sakata hilo kwa muda mrefu, huku akieleza kuwa wakati linafikia hatua nzuri wanashangaa kuona maeneo hayo yamepandwa mawe. 

"Cha kushangaza mawe yamepandwa na hata mwenyekiti wa kitongoji chetu cha Makurunge hana taarifa, huu ni uhuni, cha kushangaza viongozi wetu wameshindwa kutupatia taarifa," alieleza Miraji. 

Mzee maarufu Mussa Iddi alisema kuwa, alikuwepo eneo hilo tangu mwaka 1953, ambapo alisoma shuleni hapo, hivyo historia ya hapo anaijua vizuri na kupitia wazazi wao walidai uhuru wa Tanzania. 

"Naomba eneo hili lipimwe hatimae kuwe na huduma za kijami zitazoweza kuwa na makazi ya watu, huduma za kijamii kwa kufuata utaratibu wa urasimishaji ardhi kisheria," alisema Mzee hiyo. 

Akizungumza na waandishi baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Wasaka Mnane, alisema eneo hilo lipo na kwamba, serikali inalotambua kinachotakiwa ni kufuata taratibu za urasimishaji ardhi. 

"Nashangaa kuona baadhi ya maeneo yamepandwa mawe ambayo nikiwa mwenyekiti siyatambui kwani, yamepandwa kinyume cha taratibu," alisema Mnane. 

No comments:

Post a Comment