Sunday, September 14, 2025

Winde yatenga maeneo ya viwanja vya michezo

Kiongozi wa wakazi wa Winde, Makurunge wilayani Bagamoyo, Jafar Mwingereza

Na Omary Mngindo, Makurunge

WAKAZI wa eneo la Winde lililopo Kitongoji cha Mkwajuni Kata ya Makurunge Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameandaa eneo Maalumu litalotumika kwa ajili ya viwanja vya michezo.

Hatua hiyo imefikiwa na wakazi hao katika mkutano wa kujadili maendeleo kwenye eneo lao, lenye ukubwa wa ekari 6,000 ambalo wamelirithi kutoka kwa wazee wao walioishi miaka ya 1,532.

Hayo yamebainishwa na kiongozi wa wana Winde, Jafar Mwingereza, ambapo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hatua hiyo inalenga kuwapatia fursa wakazi wa eneo hilo kuonesha vipaji vyao.

Alisema kwamba, wanatambua umuhimu wa michezo ambayo pia imo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo katika kuiunga mkono ilani hiyo, katika mipango miji wametenga maeneo kwa ajili ya viwanja hivyo.

"Katika kuiunga mkono ilani chini ya Mwenyekiti wetu ambaye pia ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wana Winde tunaunga mkono mipango miji yetu kwa kuandaa maeneo kwa ajili ya viwanja vya michezo, lengo ni kutupatia  muda wa kujionea burudani," alisema mwenyekiti huyo.

Kwa upande wao wakazi wa Winde, Mwanabiti Hassan na Rustica Tembele, walisema hatua hiyo inakwenda kuendeleza mji wao kupitia sekta hiyo michezo mbalimbali itachezwa.

"Mpango uliopo ni mzuri kwani katika sekta ya michezo watu kutoka maeneo mbalimbali wanafika hivyo kufahamiana, hivyo kuongeza hamasa kwa jamii, tunaunga mkono mpango huo," alisema Rustica.



No comments:

Post a Comment