Header Ads

ad

Breaking News

JKCI yapewa jukumu kuu kuinua huduma za moyo barani Afrika

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia zawadi Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Generali Mathew Edward Mkingule wakati mkutano na waandishi wa habari jana mjini Lusaka kuhusu kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).

Na Mwandishi Maalumu, Lusaka

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepewa wito wa kutumia utaalamu wake wa kibingwa kuendeleza hospitali mbalimbali barani Afrika zinazotoa huduma za matibabu ya moyo, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa bara hilo kupata huduma za matibabu nje ya Afrika na kuimarisha uwezo wa ndani wa kuhudumia wagonjwa.

Rai hiyo imetolewa jana jijini Lusaka na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Generali Mathew Edward Mkingule wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa JKCI  kwa kushirikiana na  Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).

Luteni Generali Mkingule alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) ni wakati wao sasa kushirikiana na kugawana ujuzi walionao kwa maslahi ya nchi zao na Afrika kwa ujumla.

“Afrika tunayoitaka ni ile ya mshikamano na ushirikiano, tusishindane bali tushirikishane na kubadilishana uzoefu, ujuzi na umahiri wetu kwa ajili ya ustawi wa watu wetu na maendeleo ya Afrika kwa ujumla,”alisema Luteni General Mkingule.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia zawadi Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Dkt. Chabwela Shumba wakati mkutano na waandishi wa habari jana mjini Lusaka kuhusu kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).

Aidha, Luteni General Mkingule alisema Serikali ya nchi hizo mbili inatambua na kuthamini kwa dhati msaada wanaopata kutoka nje ya nchi hususan kutoka Shirila la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel kwani, watoto hawana mipaka haijalishi wapo Afrika hivyo ni vizuri wakasaidiwa kwa pamoja na kuokoa maisha yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, alisema JKCI na NHH wamesaini makubaliano mwaka 2023 kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa bobezi za matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya kambi maalumu za upasuaji wa moyo angalau mara mbili kwa mwaka.

“Tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo JKCI imeshatoa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kwa wauguzi 14 kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia, huku wanne wakiendelea na mafunzo hayo sasa.”

“Tumeshafanya kambi maalumu za upasuaji wa moyo kwa watoto nne katika hospitali hii kwa kushirikiana na SACH na wadau wengine wa kimataifa, na kwa sasa timu yetu ipo hapa kwaajili ya kambi maalumu ya tano. Takriban wananchi wa Zambia 100 wamepata huduma kupitia ushirikiano huu, ambapo kati yao asilimia 43 walifanyiwa upasuaji wa moyo,” alisema Dkt. Kisenge.

Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Lusaka wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).

Dkt. Kisenge alisema kwa kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake JKCI imekuwa miongoni mwa Taasisi inayotoa huduma bingwa na bobezi za matibabu ya moyo Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara hivyo inatamani kuona Taasisi nyingine zinazotoa huduma hiyo hususani za umma zinapata mafanikio ambayo taasisi hiyo imepata.

Naye, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Dkt. Chabwela Shumba alisema JKCI na SACH ni Taasisi mbili za kipekee zilizoamua kuungana kwa pamoja kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Zambia.

Dkt. Shumba alisema katika kambi hiyo wataalamu hao wanafanya upasuaji wa moyo wa kisasa kwa watoto ambao wataalamu wa Hospitali hiyo wasingeweza kufanya hivyo ingepelekea watoto hao kupelekwa nje ya Zambia kwaajili ya matibabu.

“Katika kambi hii tumewafanyia uchunguzi watoto zaidi ya 30 ambapo watoto 10 watafanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na watoto 20 watafanyiwa upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo wa Cathlab," alisema Dkt. Shumba.

Mkurugenzi Mtendani wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Lusaka wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akielezea namna wanavyoshirikiana na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) kuwachunguza watoto wenye magonjwa ya moyo wakati na mkutano na waandishi wa habari jana mjini Lusaka kuhusu kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayoafanyika katika Hospitali ya NHH iliyopo Lusaka nchini Zambia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Dkt. Chabwela Shumba alipotembelea chumba cha uangalizi maalumu (ICU) wakati wa kambi maalumu ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Dkt. Chabwela Shumba na Mkurugenzi wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel, Samweli Fisher wakiunganisha mikono kuonyesha ushirikiano wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanyika katika Hospitali ya NHH iliyopo Lusaka nchini Zambia. Picha zote na JKCI


No comments