Mwenyekiti UWT Ruangwa ajitosa udiwani viti maalum
Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paulina Mmuya, akionesha fomu aliyochukua ya kuwania udiwani viti maalum Jimbo la Ruangwa. Mwingine ni Katibu wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho Wilaya ya Ruangwa, Fatuma Malindi
MWENYEKI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Paulina Mmuya, amejitosa kuwania nafasi ya udiwani viti maalum katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba Mwaka huu.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Paulina amesema kuwa, anataka kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Ruangwa katika nafasi ya udiwani.
Amesema kuwa, amewahi kuhuduma kama diwani wa viti maalum wilayani Ruangwa kwa muda wa miaka minne kuanzia mwaka 2015 hadi 2018 kupitia Chama cha wananchi (CUF), lakini aliachana na chama hicho na kujiunga na CCM mwaka 2019.
Paulina amesema kuwa, baada ya kujiunga na CCM, aliamua kuwania nafasi ya uenyekiti wa UWT Wilaya ya Ruangwa na kufanikiwa kushinda nafasi hiyo ambayo anaitumikia hadi hivi sasa.
"Nilianza siasa nikiwa kijana sana, baada ya kutoka CUF na kujiunga na CCM, niliaminiwa kutokana na utendaji wangu wa kazi na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa UWT Ruangwa, hivyo nikipewa ridhaa ya kuwa diwani viti maalum, nitaitendea haki nafasi hii," amesema.
Paulina amesema kuwa, sera nzuri za Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, zimezidi kumsukuma kuwania nafasi hiyo ili akashirikiane na viongozi wengine kuunga mkono jitihada za mwenyekiti za kusimamia maendeleo ya nchi.
Amesema Ruangwa chini ya Mbunge Kassim Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu, imefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo kuanzia miundombinu, maji, elimu, kilimo, afya na umeme.
"Majaliwa amekuwa nguzo muhimu sana kwa maendeleo ya Jimbo la Ruangwa, mambo mengi tuliyokuwa tukiyapigia kelele kabla ya kuingia madarakani kwa mbunge wetu, alihakikisha anayapigania na kufanikiwa kuyatekeleza," amesema.
Ameongeza kuwa, kama chama chake kikimpa nafasi hiyo atahakikisha anasimamia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025, kwa manufaa ya wilaya ya Ruangwa.
No comments