Header Ads

ad

Breaking News

Rais Samia apokea gawio la shilingi trilioni 1.028

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali kwenye hafla ya kupokea Gawio la Serikali iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Juni 10,2025


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa mashirika na taasisi za umma kuhakikisha yanawajibika kulinda na kuendeleza uwekezaji wa serikali kwenye mashirika hayo, pamoja na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu, imesema Dkt.Samia ametoa wito huo leo Jumatano Juni 10,2025 katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika taasisi na mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina hisa zake.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amesema kuwa, mageuzi makubwa yanayotekelezwa na serikali katika usimamizi na uendeshaji wa mashirika ya umma yameonesha mafanikio,  mashirika 11 kati ya 13 yaliyokuwa na mtaji hasi kwenda kwenye kundi lenye mtaji chanya, wakati mashirika nane kati ya hayo yaliyokuwa yakipata hasara, kwasasa yameanza kupata faida.

Rais Dkt. Samia amemwagiza Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kuendelea kuwajengea uwezo watendaji kwa lengo la kuhakikisha mashirika hayo yanaongeza ubunifu ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA.

Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa kutambua mashirika na taasisi ambazo hazitoi mchango wa fedha moja kwa moja kwa serikali, lakini huchangia kupitia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.


Serikali imepokea gawio la jumla ya Shilingi trilioni 1.028 kutoka mashirika na taasisi za umma ikiwa ni ongezeko la asilimia 34, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 767 zilizotolewa mwaka jana.

Pia, idadi ya taasisi na mashirika na yaliyochangia imeongeza kufikia 213, wakati kampuni zenye hisa chache za serikali zikiwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa, ikiwemo Twiga Minerals iliyochangia Shilingi bilioni 93.6, Airtel Tanzania Shilingi bilioni 73.9 na NMB Bank Shilingi bilioni 68.1.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, akizungumza wakati wa kupokea gawio
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko, akifuatilia matukio mbalimbali
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akifuatilia matukio mbalimbali









No comments