NHC yayapata faida Sh.bilioni 235.4, yatekeleza maagizo ya Rais, Dkt. Samia
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Hamad Abdallah Hamad, amesema katika kipindi cha miaka mitano (2019/20 – 2023/24), Shirika limepata faida ya Sh. bilioni 235.4, wakati ukuaji wa faida kwa miaka mitano ukiwa asilimia 33.1.
Amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024, Shirika limepata faida kabla ya kodi ya Sh. bilioni 36.8 sawa na asilimia 112.5 ya lengo kwa hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, mtaji wa Shirika hadi kufikia Juni 2024 ulikuwa Sh. trilioni 5.5, ikilinganishwa na mwaka uliopita ambao mtaji huo ulikuwa Sh. trilioni 5.08.
"Katika miaka mitano (2019/20-2023/24), mapato ya Shirika yamekua kutoka Sh. bilioni 125 kwa mwaka hadi Sh. bilioni 189 sawa na asilimia 34. Mapato ya mwaka 2023/24 ambayo yamekaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali yamefikia Sh. bilioni 189."
Kuhusu kodi na magawio yaliyolipwa serikali, amesema katika kipindi cha miaka mitano(2019/20-2023/24) Shirika limelipa kodi mbalimbali serikalini zinazofikia Sh. bilioni 134.4, ambapo katika kipindi hicho cha miaka mitano (2019/20- 2023/24), Shirika lililipa Gawio kwa Serikali Sh.bilioni 9.85. Mwaka huu pekee 2025 Shirika limelipa gawio la Sh. bilioni 5.5.
Amesema katika katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Shirika limejenga nyumba 5,399 zenye thamani ya shilingi bilioni 659.48 kwa ajili ya kuuza na kupangisha, ambapo nyumba 3,217 ujenzi wake umekamilika na nyumba 2,182 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2026.
Kuhusu miradi ya ukandarasi, amesema Shirika limetekeleza miradi 67 ya ukandarasi yenye thamani ya Shilingi bilioni 458.2 ambapo ujenzi wa miradi 57 umekamilika na miradi 10 ujenzi upo katika hatua mbalimbali.
"Miradi iliyokamilika kwa asilimia kubwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya ofisi za wizara nane (8) za Serikali eneo la Mtumba, asilimia 95; Soko la Kimataifa la Madini ya Tanzanite Mirerani- asilimia 96; Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) asilimia 100; Ghala la Chakula Masasi Vijijini asilimia 100 na miundombinu kwa ajili ya tanuru (incinerator) la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) eneo la Nala jijini Dodoma limefikia asilimia 100."
Wahariri wakisiliza kwa makini wasilisho
Mkurugenzi amesema kuwa, Shirika linaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nyumba za makazi ukiwemo mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati chini kupitia mradi wa Samia Housing Scheme (SHS), ambao utekelezaji wake unaendelea.
"Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha, unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba bora nchini, asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika Mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine."
Amezungumzia ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, ambapo nyumba 560 zimejengwa katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam na kuuzwa na sasa Shirika lipo katika hatua ya kuanza kukabidhi nyumba hizo kwa wanunuzi asilimia 91 na gharama bilioni 48.
Aidha, mradi huo wa nyumba 5,000 unaotekelezwa kwa awamu, utagharimu takriban Sh. bilioni 466 sawa na Dola za Kimarekani milioni 200, wakati awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo imeanza eneo la Medeli jijini Dodoma na Kawe na Kijichi jijini Dar es Salaam, ambapo nyumba 908 zinajengwa, wakati ujenzi wa nyumba 68 Iyumbu zimekamilika kwa asilimia 100.
Amesema kwa upande wa ujenzi wa nyumba za biashara, wanajenga Jengo la Biashara Masasi mkoani Mtwara ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75, Jengo la Biashara mkoani Morogoro (2H), ujenzi umefikia asilimia 80 na Jengo la Biashara Mtanda limefikia asilimia 54.
"Miradi ya kimkakati iliyopo Mount Meru (Arusha), Tabora Commercial Complex (Tabora), Singida Shops (Singida), Kashozi Complex (Kagera), Mkwakwani Plaza (Tanga), Uluguru Plaza (Morogoro), Iringa Commercial Complex (Iringa), maghala ya biashara(Mtwara) na maduka ya biashara Ilala jijini Dar es Salaam, ujenzi wake umeanza.
Maafisa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na wahariri wakiwa makini kusikiliza wasilisho
Kuhusu miradi mikubwa iliyosimama, amesema kazi ya ukamilishaji wa miradi iliyosimama tangu 2018 inaendelea, ambapo Mradi wa Morocco Square, mmoja kati ya miradi mitatu mikubwa ya makazi iliyokwama kuanzia mwaka 2018, sasa umekamilika na nyumba zake 100 zimeuzwa kikamilifu, maeneo ya biashara na ofisi yamepangishwa kwa umma.
Amesema ufanisi huo umewezekana baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kutoa kibali cha kukopa Shilingi bilioni 174 mwaka 2023 na kuukwamua mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni 153, wakati ujenzi wa Mradi wa Kawe 711 wenye thamani ya shilingi bilioni 169 umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026.
"Natoa shukrani za dhati kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Shirika la Nyumba la Taifa kupata kibali cha kukopa shilingi bilioni 174 mwaka 2023. Fedha hizi zimesaidia kukamilisha Mradi wa Morocco Square uliokuwa umesimama kwa miaka mitano na kuanza ujenzi wa KAWE 711," amesema.
"Mradi wa Golden Premier Residence (GPR) wenye thamani ya Shilingi bilioni 127 uliopo Kawe, mazungumzo kati ya mkandarasi na Shirika yamekamilika na ujenzi unaendelea na utakamilika Septemba 2027."
Ameongeza kuwa, mradi wa Plot.300 Regent Estate, uliokuwa umesimama kwa muda na sasa wameutangaza ili kupata mkandarasi wa kuendelea na ujenzi, hatua inayolenga kurejesha utekelezaji wa mradi huo uliokuwa umesimama tangu mwaka 2018, ili kuchochea maendeleo ya eneo la Regent Estate na Jiji kwa ujumla.
"Usimamizi wa ujenzi soko la Kariakoo wenye thamani ya Sh. bilioni 28 umekamilika kwa asilimia 100. Mradi huu umeshakabidhiwa kwa Shirika la Masoko Kariakoo na usanifu na usimamizi wa Jengo la Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango eneo la Mtumba umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 92 na Mjenzi ni Kampuni ya Estim Construction."
Amesema usimamizi wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), umefikia asilimia 90 na mjenzi ni Suma JKT, usanifu na ujenzi wa Jengo la Soko la Madini (Tanzanite) eneo la Mirerani Manyara ambalo usanifu wake umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 96.
Ameongeza kuwa, kutokana na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufungua uchumi wa nchi na kushirikisha sekta binafsi ambayo ni injini ya maendeleo endelevu, Shirika lilifanya marekebisho ya Sera ya Ubia ambayo ilizinduliwa rasmi Novemba 16, 2022 jijini Dar es Salaam, sera ambayo imechochea ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa majengo ya matumizi mbalimbali, ambapo jumla ya miradi 21 yenye thamani ya shilingi billioni 351 inaendelea kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam (17), Mwanza (3) na Iringa (1).
"Shirika limeidhinisha miradi mingine 64 yenye thamani ya shilingi bilioni 607 na uchambuzi wa uwezo wa wawekezaji hao unaendelea kabla ya kupewa mikataba.
Utekelezaji wa miradi hii una manufaa makubwa ikiwemo kuongeza upatikanaji wa nyumba bora za makazi na biashara, kuongezeka kwa ajira kwa watanzania na kupendezesha mandhari ya miji yetu na wigo wa kodi na mapato ya Serikali."
Amesema NHC imeendelea kufanya vikao na wapangaji wa eneo la Kariakoo na wamepisha wabia kufanya uendelezaji unaokusudiwa, wakati wapangaji waliokuwa wakilipa kodi vizuri wamehakikishiwa kurejeshewa upangaji wao pindi ujenzi wa majengo mapya utakapokamilika.
Mkurugenzi huyo amesema Shirika limepunguza madeni yake kutoka shilingi bilioni 27 hadi 22 baada ya kukusanya bilioni 5. Jitihada hizi zimewezekana kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kukusanya madeni ya serikali.
Amesema ili kukabiliana na changamoto za madeni, kampeni ya kukusanya kodi na malimbikizo kutoka kwa wadaiwa sugu, imeendelea kwa kutumia mikakati ya kuchukua hatua kwa wadaiwa wasiozingatia masharti ya mikataba, ambapo wapangaji 150 wamevunjiwa mikataba yao.
Vilevile, Shirika linashirikiana na NIDA, Credit Information Reference Bureau na BRELA ili kuwapata wadaiwa wengine binafsi na kampuni zilizohama kwenye nyumba za Shirika, pia limewapa notisi wadaiwa 100 ya kuhakikisha wanalipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
"Wapangaji wote wa sasa na wa zamani wamelipa amana ya pango, tuna amana zinazofikia Sh. bilioni 27."
"Tunaendeleza miji midogo ndani ya mji mkubwa (Satellite Towns) ya Luguruni wilayani Ubungo), Salama Creek wilayani Kigamboni), Kawe wilayani Kinondoni), Safari City Arusha Jiji na eneo la Usa River wilayani Meru," amesema.
Amezungumzia matengenezo ya nyumba kwamba, hadi Mei 15, 2025, Shirika limekarabati na kuboresha nyumba 3,004 zilizopo kwenye majengo 205, linafanya ukarabati wa nyumba 1,546 zilizopo kwenye majengo 45 unaendelea katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema ukarabati huu ni endelevu na nyumba zote za Shirika zinatarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa ifikapo 2026/27.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa, ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani, mwanzoni mwa mwaka 2021, Shirika lilianza kutengeneza mfumo jumuishi “NHC Integrated System – NHC IS”, mfumo huo ulitengenezwa na wataalamu wa nchini, wakisimamiwa kwa karibu na Kitengo cha TEHAMA cha Shirika.
Amesema mpaka sasa mfumo huo unawasiliana na mfumo wa malipo wa GePG na mfumo wa TRA kwa ajili ya taarifa za kodi ya ongezeko la thamani, na wanategemewa mfumo huo utaendelea kuunganishwa na mifumo mingine kadiri itakavyohitajika ili kurahisisha kazi za Shirika na kutoa huduma kikamilifu.
"Shirika linakamilisha mfumo wa NHC MOBILE APP utakaowezesha wateja kuwasilisha maoni na mambo mbalimbali ya kuboresha huduma za Shirika kwa kutumia simu za mkononi. Mfumo huu utakuwa tayari ifikapo Julai 2025."
Amesema zimekuwepo juhudi mbalimbali za kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na usimamizi madhubuti wa miradi ya ujenzi. Juhudi hizi zimeendelea kupunguza gharama za uendeshaji wa Shirika na kuliongezea Shirika mapato stahiki.
Ameongeza kuwa, ili kudhibiti matumizi katika miradi, Shirika limeweka kamera (CCTV) katika miradi yote mikubwam wamefunga vifaa vya bayometriki (biometric fingerprint) ili kudhibiti malipo ya wafanyakazi katika miradi mikubwa ya Shirika. Hatua hizi zimeongeza tija na faida kwa Shirika.
"NHC tulitunukiwa tuzo ya Mjenzi Bora wa Makazi ya Umma kwa Mwaka 2024 na Taasisi ya Global Construction, tulitunukiwa tuzo na NBAA ya Uandaaji Bora wa Hesabu wa Mashirika ya Umma kwa kufuata Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu(IFRS) na kushinda Tuzo ya Mjenzi Bora wa Makazi ya Kuishi Afrika Mashariki kwa mwaka 2024(East Africa Construction Awards)."
Amezitaja tuzo nyingine ni ya Mkandarasi Bora wa Makazi ya Kuishi, Tuzo za ZICA 2025 katika Tuzo za Kimataifa za Ujenzi Zanzibar (Zanzibar International Construction Awards (ZICA), cheti cha kutambua udhamini wake katika Mkutano wa 13 na 14 wa wahariri jijini Dodoma na Songea, kwa kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kueneza mafanikio ya serikali.
Amesema Shirika limeendeleza utekelezaji wa sera ya huduma kwa jamii (CSR) kwa kutoa michango katika sekta za elimu, afya, vijana, maendeleo ya jamii na michezo.
Katika kipindi cha miaka mitano(2020-2024) Shirika limetoa misaada kwa jamii ya Sh. bilion 1.42.
"Mwelekeo wa Shirika ni kuanzisha NYUMBANI BOND ambayo itawezesha watanzania kununua hisa na hivyo kutunisha mapato ya Shirika ili liweze kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali nchini. Kujenga miradi ya kimkakati ili kukidhi mahitaji ya nyumba za biashara na Ofisi katika maeneo mbalimbali nchini na kuendelea na ujenzi wa nyumba 5,000 za Samia Housing Scheme eneo la Medeli, Mtoni Kijichi, Kawe 711 na Iyumbu."
No comments