Rais Mwinyi azitaka taasisi za umma kutekeleza sera ya biashara
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameagiza taasisi za umma kutekeleza sera ya biashara (Zanzibar Trade Policy) na Ripoti ya Tathmini ya mazingira ya ufanyaji biashara (Zanzibar blue Print), ipasavyo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Biashara ya mwaka 2024 na ripoti ya tathmini ya mazingira ya ufanyaji biashara ya mwaka 2024 na mpango kazi wa utekelezaji wa Sera na Ripoti ya Tathmini, Zanzibar.
Kuzinduliwa kwa sera hizo kutaweka mazingira rafiki na rahisi ya ufanyaji biashara na ukuzaji wa sekta ya biashara nchini, na kwamba serikali, itatekeleza, kuendeleza na kusimamia sera hizo pamoja na kuzifanyia kazi.
“Nazitaka mamlaka za utoaji leseni na mamlaka za usimamizi kuchukua hatua za haraka katika maeneo yote ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kurahisisha ufanyaji biashara na kuweza kufikia malengo ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050, na malengo ya mpango wetu wa maendeleo wa mwaka 2020/2021- 2025/2026."
Ameipongeza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia maendeleo ya sekta ya biashara na viwanda ili kuhakikisha biashara inafanyika kwa urahisi na bila urasimu, pamoja na kuhakikisha mazingira mazuri ya uwekezaji katika biashara na viwanda yanazingatiwa.
“Vitabu hivi vinategemewa sana katika kukuza sekta ya biashara kwani vitawasaidia wafanyabiashara kupata uelewa kuhusiana na mazingira ya ufanyaji biashara na kuzisaidia taasisi kujitathmini kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini,”amesema.
Amesema uandaaji wa sera mpya ya biashara na tathmini ya mazingira ya ufanyaji biashara ni hatua ya kufanikisha ahadi ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 ibara ya 157 inayoitaka serikali kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara.
Amesisitiza kuwa, Sera ya biashara ya mwaka 2024 ni matokeo ya mapitio ya Sera ya Biashara ya mwaka 2006.
Amesema sera hiyo mpya imelenga kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa na uwanja mpana wa kufanya biashara zao kiushindani na kushiriki vizuri katika kufanya biashara kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza ushindani wa mauzo nje ya nchi ili kuongeza wigo wa bidhaa kufikia masoko mapya.
Ameongeza kuwa, ripoti ya tathmini ya mazingira ya ufanyaji biashara (Zanzibar Blue Print) iliyoandaliwa mwaka 2024, ina lengo la kuimarisha biashara na kuondoa urasimu.
“Tathimini hii imeweka mapendekezo ya kutatua changamoto katika makundi matatu makuu ambayo ni sera zinazohusiana na biashara, sharia na taasisi zinazosimamia biashara,”amesema.
Kwa upande wa taasisi zinazosimamia biashara, amesema ripoti hiyo imetoa mapendekezo ya kuondoa mwingiliano wa majukumu ya kiutendaji katika taasisi zinazohusiana na usimamizi wa biashara na majukumu ya mamlaka za udhibiti, kuwepo kwa utaratibu wa pamoja wa utoaji wa leseni, vibali na ada katika biashara, utalii, uwekezaji na usafirishaji.
Amependekeza kuanzisha mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi zinazosimamia masuala ya biashara katika kutoa huduma na kutoa vibali vya kazi kwa wageni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara.“Sera na ripoti hii ilipita serikalini na sisi tulipata fursa ya kuisoma na kuikubali."
“Niwaombe wadau kutoka sekta binafsi na washirika wa maendeleo tuendelee kushirikiana katika hatua zote za utekelezaji wa sera hii na kutekeleza mikakati maalum ya ukuzaji wa biashara kwa lengo la kukuza biashara hapa Zanzibar,”amesema.
Amesema ni faraja kwa serikali kupata mafanikio makubwa na ya kujivunia katika kuendeleza sekta ya biashara.
No comments