Rais Dkt.Mwinyi awataka wafanyakazi kuendelea kutekeleza majukumu yao
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wafanyakazi wote nchini, kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, maarifa, uadilifu na uzalendo na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele.
Pia, kwa vyama vya wafanyakazi, kushirikiana na serikali na waajiri ili kuhakikisha wanaongeza tija kwenye maeneo yao ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 1,2025 wakati akitoa hotuba ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Zanzibar.
Amesema kuadhimisho siku hiyo ni ishara ya ushirikiano uliopo kupitia utatu baina ya serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi, jambo ambalo limewezesha kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi hapa nchini.
“Wito wangu kwenu nyote tuendelee kuimarisha ushirikiano huu kwa faida ya pande zote ili uwe chachu ya kuleta maendeleo zaidi katika nchi yetu,”amesema.
Kupitia maadhimisho hayo, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wafanyakazi wote nchini na kuwashukuru kwa juhudi zao katika kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo yao ya kazi.
Ameongeza kuwa, ni dhahiri juhudi hizo za pamoja zimewezesha kuimarisha ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma mbalimbali na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya Taifa Tanzania.
“Kwa hakika mafanikio ambayo nchi yetu inaendelea kuyapata katika sekta zote, yanatokana na juhudi zinazofanywa na wafanya kazi kwa kutimiza wajibu wao na kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo,”amesema.Amesema serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa na nzuri inayofanywa na watumishi wote na hivyo itaendelea kuchukuwa hatua za kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuzifanyia kazi changamoto ziliopo hatua kwa hatua.
Amefafanua kuwa, serikali inatambua kazi kubwa na muhimu inayofanywa na vyama vya wafanyakazi kama wadau muhimu wa maendeleo.
Ameviomba vyama vya wafanyakazi na Jumuiya za Waajiri kusaidiana na serikali katika kusisitiza ufanisi wa kiutendaji miongoni mwa wanachama wao kwa kutimiza wajibu wa kila mmoja miongoni mwao.
“Nasema hivyo kwa kutambua kuwa, bado kuna watumishi wachache wasio waadilifu ambao hawazingatii utumishi bora na wameweka mbele maslahi yao binafsi. Lazima watumishi wa aina hii wabadilike ili wasiwe kikwazo cha kuleta ufanisi katika kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo zaidi."
Ameahidi kuwa, serikali kwa upande wake itaendelea kuchukuwa hatua za kuhakikisha watumishi wanapata haki zao na stahiki zao kwa mujibu wa sheria za utumishi na kanuni ziliopo.
Amezungumzia maagizo aliyotoa Mei Mosi mwaka 2024, ya kuitaka Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kukaa pamoja na wadau wake wa utatu ambao ni vyama vya wafanyakazi na Jumuiya za Waajiri ili kujadili changamoto za wafanyakazi na kuzitafutia ufumbuzi, zimefanyiwa kazi.“Nimefarajika kuelezwa kwamba, kwa sasa vikao vitano vya wadau ambao ni Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kupitia Kamisheni ya Kazi, ZATUC na ZANEMA tayari vimefanyika na hoja 16 zimejadiliwa."
“Nimeambiwa pia majadiliano hayo yamejumuisha Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Mfuko wa Huduma ya Afya na wadau wengine."
“Tayari hoja sita zimepatiwa ufumbuzi, tano za ZATUC na moja ya ZANEMA na hoja saba zinaendelea na hatua za kutatuliwa. Ni matarajio yangu kuwa hoja zilizobaki nazo zitafanyiwa kazi na kumalizika,”amesema.
Amesisitiza mwendelezo wa vikao hivyo vya wadau ili kuzidi kupunguza changamoto zilizopo katika sehemu za kazi na kumpa taarifa ya kila hatua za utatuzi wa changamoja hizo.
Amesema kuwa, serikali imeendelea kuchukuwa hatua za kuboresha maslahi ya watumishi wake kwa namna mbalimbali, ikiwemo kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara, kuwa na mfuko wa huduma ya afya kwa wafanyakazi wake, pamoja na kushughulikia marekebisho ya maslahi ya watumishi, baada ya kuibuka kasoro za malipo yao kufuatia kuanza kutumika ongezeko la mishahara ya wafanyakazi.“Imani yangu ni kuwa, hatua hiyo imezidi kuchochea ari ya watumishi katika kada zote kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,”amesema.
Amezungumzia Uchaguzi Mkuu, Rais Dkt. Mwinyi amewataka wafanyakazi wote, viongozi, waajiri, na wananchi kwa jumla tushiriki kwa amani na kuheshimu sheria. “Tuendelee kuwa walinzi wa amani yetu kama tunavyolinda maslahi yetu kazini.
“Naomba vyama vya wafanyakazi, waajiri na wafanyakazi wote kwa ujumla, tushirikiane katika kuhamasisha kuilinda na kuidumisha amani tuliyonayo na tushiriki katika upigaji kura kwa usalama na utulivu. Tuendelee kufanya kazi kwa bidii, na tuendelee kujenga taifa lenye haki, usawa, na maendeleo kwa maslahi na mustakabal mwema wa nchi yetu,”amesema.
Aidha, kauli mbiu ya mwaka huu inasema: Wafanyakazi Tufanye Kazi kwa Bidii na Nidhamu, Tudai Haki Zetu kwa Mujibu wa Sheria na Tushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa Amani.
No comments