Mipango ya ununuzi ya sh.trilioni 46.8 yatangazwa NeST
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi (hawapo pichani), kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina,
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MIPANGO ya ununuzi ya mwaka yenye thamani ya Sh trilioni 46.8, imetangazwa kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) tangu kuanza kwa mfumo huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema hayo jana Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kati ya PPRA, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari, kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mbali na kuwezesha utangazaji wa mipango hiyo ya ununuzi, Simba amesema pia matumizi ya mfumo huo wa NeST, yameokoa fedha nyingi kiasi cha sh. bilioni 13.33 za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, ambazo zingetumika katika ununuzi wa karatasi tu kwa ajili ya maandalizi na ukamilishaji zabuni.
"NeST ni mfumo ulioundwa na wazawa ambao ni mbadala wa mfumo wa awali wa manunuzi ya umma uliokuwa ukijulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS)," amesema.
Amesema kuwa sehemu yoyote inayohusisha matumizi ya fedha nyingi, ni lazima iwe na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha uwajibikaji kwa wanaotoa huduma au bidhaa katika taasisi za umma.
Simba amesema mfumo wa NeST wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao unaosimamiwa na PPRA chini ya Wizara ya Fedha, una lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa ununuzi wa umma kupitia teknolojia mpya.
Ameongeza kuwa, mfumo huo ulioanza kutumika rasmi Julai 1,2023, ulizunduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,Septemba 9,2024, ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, katika Kongamano la Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki lililofanyika jijini Arusha.
Amesema mfumo huo umepunguza muda uliokuwa ukitumiwa na taasisi nunuzi kupata taarifa za wazabuni, hata kuchangia kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa uchakataji zabuni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa HazinaMkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, kuanza kutumika kwa mfumo huo wa NeST inakadiriwa kuwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, utafiti wa awali uliofanywa na mamlaka umebaini kuwa, mfumo huo umesaidia kupunguza Tani 617.85 za utoaji wa kaboni angani.
Amesema kuwa, katika taasisi nunuzi zote, jumla ya tasisisi nunuzi 57,993 zimesajiliwa katika mfumo wa NeST zikiwa na watumiaji 117,900 waliosajiliwa, na kwamba taasisi kuu na kasimiwa 1,215 na taasisi za ngazi za chini za serikali za mitaa 56,778, huku watumiaji 53,584 wakisajiliwa kama wasimamizi wa zabuni.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema utekelezaji mzuri wa ununuzi wa umma unahitaji kuwa na mamlaka madhubuti ya kusimamia watoa huduma na wanunuzi kutoka taasisi mbalimbali, ili shughuli hizo zifanyike kwa ufanisi na kuchochea maendeleo ya haraka.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeamua shughuli zote za ununuzi wa umma zifanyike kwa njia ya kidijitali kutokana na changamoto za mfumo wa kawaida wa manunuzi.
Afisa Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma Ofisi ya Msajili wa Hazina, Alex Nelson Malanga akizungumza katika kikao kazi hichoSimba amesema kwamba, Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 imeipatia PPRA mamlaka ya kusimamia mfumo wa ununuzi kwa njia ya mtandao (e-Procurement) ili kurahisisha na kuharakisha uchakataji wa zabuni zote za umma kupitia mfumo huo.
Amesema lengo kubwa la Serikali, ni kuboresha ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao kwa kuongeza uwazi, kupunguza gharama, kuzuia mianya ya rushwa na muda wa mchakato, ikiwemo kuimarisha ushiriki wa wazabuni wa ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi huyo amesema hadi sasa wazabuni 33,470 wamesajiliwa katika mfumo huo, ambapo kuanzia Aprili mwaka huu, mikataba na malipo yote ya ununuzi wa umma yameanza kufanyika ndani ya mfumo huo wa kidijitali.
Ameongeza kuwa, jitihada zinaendelea kuimarisha mfumo huo kwa kuongeza moduli za ziada ikiwemo ukaguzi wa ndani na mfumo wa kupokea malalamiko kutoka kwa wazabuni, ambapo hivi sasa malalamiko yanashughulikiwa moja kwa moja kupitia mfumo kwa haraka na uwazi.
Ameongeza kuwa, mamlaka hiyo imejenga 'aplikesheni' ya simu ambayo inatumiwa na taasisi nunuzi katika ngazi za shule na vituo vya afya, vijiji/mitaa na kata, wakiwemo wazabuni katika kupata taarifa na kuomba zabuni.
Amesema lengo ni kurahisisha zoezi la ununuzi wa umma mahali popote mtumiaji alipo, na kwamba mfumo wa NeST umeunganishwa na mifumo zaidi ya 20 ya Serikali ili kufanikisha uhakiki na uhalisia wa taarifa, kubadilishana taarifa na mifumo mingine pale inapobidi.
Simba amesema kuwa, changamoto iliyopo ni upinzani wa matumizi ya mfumo mpya ambapo watumiaji wengi wa taasisi nunuzi wamekuwa na ugumu wa kubadilika kutoka kwenye mifumo ya awali, wataendelea kutoa elimu na mafunzo kwa taasisi zote ili kuongeza uelewa na kupunguza hofu ya mabadiliko.
Pia, taasisi nunuzi, hususan katika halmashauri zimekuwa na changamoto za kiufundi katika kutumia mfumo kikamilifu, lakini PPRA inashirikiana na TAMISEMI na imetoa mafunzo kwa washindi 368, ambapo kila halmashauri itatoa watumishi wawili ambao baada ya kufundishwa watatoa usaidizi wa karibu katika matumizi ya mfumo ndani ya halmashauri.
Amesema kuwa, taasisi nunuzi zilizopo katika maeneo yenye changamoto ya mtandao zinapata ugumu wa kutumia mfumo, lakini Serikali inashirikiana na UCSAF na watoa huduma wa mtandao ili kuboresha miundombinu ya TEHAMA.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Bakari Machungu akizungumza katika kikao hichoSimba amesema kuanzia Februari 1, 2025, PPRA kwa kushirikiana na TAMISEMI imewezesha mfumo wa NeST kupatikana katika mtandao wa mawasiliano wa TAMISEMI, ambapo huduma hupatikana moja kwa moja kwenye halmashauri zote nchini.
Amesema PPRA kutokana na changamoto ya wataalam wa mfumo kukosa mafunzo ya dharula, mamlaka imeendelea kushirikiana na wadau wengine wenye ubobezi kwenye maeneo na kujengea uwezo watalaamu wa ndani katika kuwa na usimamizi endelevu wenye kuleta ufanisi wa mfumo.
Ameitaja mipango yao ya baadaye kuwa ni kuanza kwa ujenzi wa moduli mbili za Mnada Mtandao (e-Auction) na Katalogia ya Mtandao (e-Catalogue)/ Market Place. Pamoja na hayo, Mamlaka inaendelea na uboreshaji wa miundombinu.
Ameongeza kuwa, kukamilisha zoezi la tafiti za bei kikomo (Price Caps) kwa baadhi ya bidhaa ambazo zitawekwa kwenye Mfumo wa NeST kwa ajili ya kutumiwa na taasisi nunuzi, ambapo bei hizo zitasaidia kupunguza changamoto kwa Serikali kununua huduma na bidhaa kwa bei kubwa zisizo na uhalisia.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Tausi Mbowe na Joseph Kulangwa, wakisikiliza wasilisho
No comments