Header Ads

ad

Breaking News

Madereva 4,563 wafaulu wapatiwa vyeti vya kuthibitishwa, wengi wachemsha mitihani LATRA,

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Saluo akiwasilisha wasilisho wakati wa kikao kazi na wahriri kilichofanyika leo Jumatatu Aprili 14,2025 jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Saluo ameanika mafanikio makubwa waliopata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, na kuelezea madereva madereva 4,563 wamethibitishwa kuendesha mabasi ya abiria kwa kupatiwa vyeti baada ya kufaulu mitihani.

Nusu ya madereva wa mabasi ya abiria nchini, wamefeli mitihani ya kuthibitishwa kazini inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), huku abiria wakijitokeza kwa wingi katika huduma mpya za mabasi ya usiku. 

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Saluo, amesema hayo leo Jumatatu Aprili 14,2025 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia mafanikio ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kilichosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), CPA Saluo amesema Mamlaka husajili madereva na baadaye kuwapatia vyeti vya kuthibitishwa.

Kwa mujibu wa CPA Saluo, vyeti hivyo hutolewa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa inayofanyika katika ofisi za LATRA za mikao yote 26 ya Tanzania Bara, ambapo hadi Machi 31,2025 madereva 33,778 walisajiliwa na taarifa zao kuingizwa kwenye kanzidata ya Mamlaka.

"Kati ya madereva hawa, madereva 8,172 wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe cha utambuzi wa dereva (i-button), ambapo madereva 4,563 walifaulu mitihani ya LATRA  kati ya 9,191 waliofanya mitihani hiyo, sawa na ufaulu wa asilimia 49.65 na kupatia vyeti vya kuthibitishwa," amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akielezea umuhimu wa vikao kazi vinavyosimamiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina

Amesema matokeo hayo yanaashiria maandilizi hafifu kwa madereva, uwoga wa mitihani unaofanyiwa kwa njia ya kompyuta, upya wa zoezi la kuthitisha madereva na kukosekana kwa utaratibu wa kujisomea ama kujiendeleza kwa madareva.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema  kwa mujibu wa kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya LATRA Sura ya 413, Mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafirishaji vinavyodhibitiwa , lengo likiwa ni kuwadhibiti madereva na kuwa na madereva wenye weledi wa kuendesha magari yanayotoa huduma za usafiri wa umma na mizigo kwa usalama.

Kuhusu huduma mpya za mabasi ya usiku alisema; "Serikali ya Awamu ya Sita iliondoa zuio la mabasi kusafiri usiku lililowekwa mwaka 1994, ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la Bajeti Juni 28, 2023, aliagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Uchukuzi, kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa mabasi nyakati za usiku.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bakari Kimwanga akifafanua jambo wakati wa kikao kazi

"LATRA ilishiriki zoezi la kufanya maandalizi ya kuanza kwa safari za usiku kwa kushirikiana na wadau wake muhimu, hasa wamiliki wa mabasi wakiwemo TABOA na ilitekeleza maamuzi ya Serikali kwa kuanza kutoa ratiba za mabasi kusafiri usiku na mchana kuanzia Oktoba 1,2023," amesema CPA Saluo.

Ameongeza kuwa, tangu kuanza kwa huduma hiyo , LATRA imeendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani katika uratibu wa huduma za usafiri wa mabasi kwa kuimarisha usimamizi wa masharti ya leseni, ikiwemo ukaguzi wa mabasi, utambuzi wa medereva kwa i-buttons na kuongeza matumizi ya VTS.

Kwa mujibu wa CPA Saluo, hadi Machi 31, 2025 mabasi 2,323 yalikuwa yamepatiwa ratiba za kutoa huduma za usafiri usiku na mchana, wakati tathmini ya LATRA ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa ruhusa ya safari za usiku na mchana, ikionesha wananchi wengi wamefurahishwa na kuridhishwa na maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuondoa zuio la mabasi kusafiri usiku.

.Mjumbe wa Kamatgi ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhariri Mkuu wa gazeti la Raia Mwema, Joseph Kulangwa akiuliza swali

"Kuna mwitikio mkubwa wa wananchi kutumia usafiri wa usiku kuliko mchana, hata msongamano wa abiria kwenye stendi umepungua na mchezo wa mabasi kukimbizana umepungua na unaelekea kumalizika kabisa. Pia zimepunguza  gharama za njiani kwa abiria na kuongeza matumizi ya muda wao kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na kujiongezea kipato," amesema. 

CPA Saluo amesema pia kuanzia Februari 2021 hadi Machi 2025, wametoa leseni 108,658 za usafirishaji.

Amezitaja leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, kukodi na mizigo, kwamba zimeongezeka kutoka 226,201 kwa mwaka 2020/2021 (Februari 2021) hadi 334,859 kwa mwaka 2024/2025 (Machi 2025).

Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, LATRA  ina wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na au kufuta leseni za usafirishaji.

CPA Saluo amesema kuna ongezeko la leseni 108,658 sawa na ongezeko la asilimia 48, hivyo ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne.

Mjumbe wa Kamatgi ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim akiuliza swali wakati wa kikao kazi hicho

Amesema pia LATRA wameanzisha njia mpya 1,007 za usafiri wa daladala mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kufika sehemu ambazo hazifikiki na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kuwapunguzia wananchi gharama.

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa, LATRA wanaendelea kuboresha usafiri katika majiji na miji mikubwa nchini ili kuwarahisishia usafiri wananchi.

Amezitaja njia za daladala Dar es Salaam zilizorefushwa kuwa ni Gerezani-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo; Buyuni Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Kinyerezi; Mbezi Luis-Kisarawe kupitia Barabara ya Malamba Mawili; Banana, Toangoma-Pugu Stesheni kupitia Barabara ya Kilwa na Nyerere na Kivukoni-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo.  

Nyingine za Dar es Salaam ni Bunju Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Madale; Mbande, Kisewe-Gerezani kupitia Barabara ya Usalama; Chang'ombe, Usalama, Mvuti-Machinga Complex na Tabata Segerea.

Njia nyingine ni Kitonga-Gerezani kupitia Barabara ya Kilwa na Ngobedi B-Machinga Complex kupitia Nyota Njema.


Mjumbe wa Kamagi ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Stella Aron, akizungumza

Kwa upande wa Jiji la Arusha, CPA Saluo amesema LATRA imefanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya kuwa za mzunguko kwa lengo kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na huduma ya usafiri huo.

Ameitaja njia inayoanzia Kwa Mrombo kupitia Impala, Phillips, Sanawari, Chuo cha Ufundi Arusha hadi 'Fire' na kurudi, wakati jijini Dodoma njia mpya zilizoanzishwa ni Machinga Cmpolex-Njedengwa; Machinga Complex-Mpamaa; Machinga Complex-Chidachi; Machinga Complex-Nzuguni; Machinga Complex-Swaswa na Vyeyula-Ilazo.

Amesema hatua ya kuhamishia daladala kituo cha Machinga Complex Dodoma, zimesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya Jiji la Dodoma na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya usafiri kwa wananchi.

Ametaja mzunguko huo ni kuanzia Barabara ya Hospitali kupitia Mjengo Sokoni hadi Machinga Complex kisha kupitia Uwanja wa Ndege na kurudi mjini.

Mkurugenzi Mkuu huyo amezitaja njia ndefu zilizoanzishwa jijini Mwanza kwa lengo la kuyafikia maeneo mapya ya makazi na kukua kwa kasi kwa jiji hilo ambazo ni pamoja na Usagara-Kisesa kupitia Buzuruga.

Zingine ni Ilalila-Misungwi kupitia Buzuruga; Nyashishi-TX kupitia Kiseke-PPF; Nyashishi-Kisesa Kona ya Kayenze kupitia Mecco; Nyashishi-Ilalila kupitia Buzuruga; Mwanza Mjini-Igombe; Mwaloni-Kona ya Kayenze na Mwaloni-Kabusungu.

Mhariri wa gazeti la Pambazuko Peter Nyanje akiuliza swali
Wahariri wakisikiliza wasilisho la mkurugenzi mkuu wa LATRA
Wahariri wakifuatilia wasilisho la mkurugenzi mkuu wa LATRA leo Jumatatu Aprili 14,2025 jijini Dar es Salaam

Wahariri wakifuatilia wasilisho la mkurugenzi mkuu wa LATRA
Mhariri Mkuu wam Habari Leo, Mgaya Kigoba akisikiliza kwa makini wasilisho


No comments